×

Walotupiga watumishi hewa nao wapigwe

Tanzania's President elect John Pombe Magufuli addresses members of the ruling Chama Cha Mapinduzi Party (CCM) at the party's sub-head office on Lumumba road in Dar es Salaam, October 30, 2015. Tanzania's ruling party candidate, John Magufuli, was declared winner on Thursday of a presidential election, after the national electoral body dismissed opposition complaints about the process and a demand for a recount. The election has been the most hotly contested race in the more than half a century of rule by the Chama Cha Mapinduzi Party, which fielded Magufuli, 56, a minister for public works. REUTERS/Sadi Said

Rais Dk. John Pombe Magufuli.

INAKARIBIA miezi sita sasa tangu Rais Dk. John Pombe Magufuli aapishwe kuwa kiongozi wa awamu ya tano wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pale Novemba 5, mwaka jana.

Kuna ambao walibeza staili ya uongozi wake mara tu baada ya kuanza kazi, wakisema ni nguvu za soda, kwani uzoefu ulionesha kila kiongozi mpya anapoingia madarakani, anakuja na mbinu zake za utawala.

Alifanya vitu vingi kwa muda mfupi, alipiga marufuku safari za nje zisizo na tija kwa watumishi wa umma, akafuta sherehe za Uhuru zilizopangwa kutumia mabilioni ya shilingi, akahimiza uwajibikaji makazini na akaziba mianya ya rushwa, akahimiza ulipaji kodi, sambamba na kukabiliana na ubadhirifu kwa nguvu zote.

Hadi tunapofikia Aprili katikati, miezi sita tangu aanze kazi yake ya urais, hakuna dalili kuwa kasi yake itapungua, kwani kila siku kumekuwa na msisitizo wa maboresho ya maagizo aliyokwishatoa, pamoja na mengine mapya ambayo yote, yanalenga kuboresha maisha na kuondoa kero za wananchi.

Kuna hii kazi mpya, ambayo wakuu wa mikoa walipewa siku 15 kuimaliza, kuhusu wafanyakazi hewa, ambao wamejazana karibu katika kila idara za serikali, hasa katika halmashauri. Wamejaa katika sekta karibu zote.
Hawa miongoni mwao ni wale waliofariki dunia, waliofukuzwa au kuacha kazi na baadhi yao, wapya kabisa ambao hawajawahi kufanya kazi sehemu yoyote.

Hadi makala haya yanaandikwa, zaidi ya wafanyakazi hewa 7,000 nchi nzima walikuwa wameshabainika, ambao kila mwezi wanalipwa mishahara ambayo inakadiriwa kufikia mabilioni ya shilingi.
Hii ni mojawapo ya kazi nzuri chini ya Rais Magufuli. Kuwabaini, kunamaanisha ni kuokoa mamilioni ya shilingi, ambazo zitaelekezwa sehemu zingine zenye uhitaji, hasa elimu na afya, ambazo zimekuwa ni kero ya muda mrefu ya Watanzania wengi wa hali ya chini.

Lakini huo ndiyo mwisho? Hapana. Zoezi hili ni refu kuliko inavyotazamwa, kwa sababu baada ya kuwabaini watumishi hawa hewa, tunahitaji kuwajua waliohusika. Yawezekana baadhi ya watendaji hawajui kama walipewa majina ya watumishi hewa!
Lakini jambo moja tulilo na uhakika nalo ni kwamba mishahara hiyo ilichukuliwa. Kama Mkurugenzi wa kitengo alipewa taarifa za uongo na yeye kulipa, ni wazi kuwa aliyedanganya ndiye aliyechukua mshahara huo.
Tunahitaji kumjua huyu aliyedanganya ili aadhibiwe kwa wizi alioufanya kwa miaka yote. Serikali inatakiwa kuwachukulia hatua kali kabisa za kinidhamu, ikiwemo kuwafungulia mashtaka na wakithibitika, licha ya vifungo, mali zao pia zifilisiwe.

Na tunataraji kuwa serikali itasogea mbele zaidi kwa kuwaadhibu pia kwa uzembe, wakubwa walioruhusu kudanganywa kwa miaka yote bila wao wenyewe kufanya uhakiki wa kujiridhisha juu ya namba ya watu wanaostahili malipo.

Huu ni mchezo wa miaka mingi katika idara za serikali, kwa sababu kila mmoja alikuwa akitafuta mwanya wa ‘kupiga’. Mbona watumishi hewa hawapatikani katika sekta binafsi?
Rais Magufuli anatakiwa kulisimamia kwa nguvu zote zoezi hili, kwani upo uwezekano akapigwa ‘changa la macho’ kama ilivyowahi kutokea huko nyuma ambapo viongozi wamekuwa wakisomewa ripoti zilizopikwa, zinazokosa uhalisia.

Wametupiga kwa muda mrefu, ni zamu yao sasa nao kupigwa ili kama watoto wa mjini wanavyosema, ngoma iwe droo. Kuna kelele tunazisikia zikiwatetea wahalifu wanaotumbuliwa na serikali ya awamu ya tano, hawa nao wanatakiwa kutazamwa huenda nao wana ‘mazabe’ yao, wanahofia zamu yao ikifika!
Nachochea tu!

Leave a Comment