×

Lowassa; muache Magufuli afanye kazi!

KWAKO Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa. Habari za majukumu ya kila siku mkuu?
Binafsi sijambo, namshukuru Mungu. Naendelea na majukumu yangu ya kila siku hapa Global Publishers, tunashikana mashati kwelikweli kuhakikisha Watanzania wanapata habari motomoto.
Nimekukumbuka mzee wangu leo. Nimekuwa na utaratibu wa kuwaandikia barua watu wenye nyadhifa mbalimbali katika jamii, leo ni zamu yako.

Madhumuni ya barua hii kwanza kabisa ni kutaka kukupongeza kwa kuonesha ushindani wa hali ya juu katika uchaguzi uliopita wa Oktoba 25, mwaka jana. Ulionesha jinsi gani una nguvu. Jinsi gani unakubalika. Maana kura ulizozipata, hazikuwahi kupatikana tangu mfumo wa vyama vingi uanze nchini.

Kupitia vyombo mbalimbali vya habari wiki iliyopita, ulinukuliwa ukikosoa utendaji kazi wa Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Pombe Magufuli. Ukajaribu kujenga hoja kwamba kinachoendelea kwa sasa ni mhemko wa Watanzania kumpata rais mpya, lakini itaisha baada ya muda mfupi na hakutakuwa na mafanikio.

“Hali ya siasa hivi sasa ni ya hamasa kutokana na serikali mpya na ‘staili’ mpya, kwa kipindi kifupi atakuwa maarufu (Magufuli), lakini hakuna mafanikio ya kiuchumi mbele ya safari,” ulinukuliwa hivyo.
Sitaki kusema kwamba ukosoaji wako ni mbaya lakini najaribu kupima na hali mbaya tuliyokuwanayo kabla, naona ni afadhali aendelee na staili hiyo unayoiita mpya.

Mkuu hii nchi ilikuwa imeoza. Watu walihalalisha maovu kuwa mema na mema kuwa ndiyo maovu. Ilifika wakati hata wale watumishi wachache waliokuwa wanataka kutenda mema, walijiona wakosaji.

Walijiona wakosaji kwa sababu kila mtu alitenda maovu. Sasa ili kuleta heshima ni bora kusafisha kabisa ‘uchafu’ wote. Nchi iligeuka shamba la bibi, kila mtu anafanya anachotaka, hakuna wa kumnyooshea mwenzake kidole.
Sasa tumepata rais anayethubu kunyosha kidole. Anayethubutu kukemea vitendo vya rushwa na ufisadi. Tena si kukemea tu, anataka kuona anayetenda kosa anawajibishwa bila kuangalia wadhifa wake.
Nimeshangazwa zaidi pale uliposema eti rais anakosea pia anapogawa fedha zilizotengwa kwa ajili ya sherehe fulani na kwenda kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, kwamba jukumu hilo ni la taasisi kama bunge. Kwa nini tusubiri Bunge wakati nchi ina hali mbaya?
Watanzania ni mashahidi, kila fedha ya sherehe iliyofutwa inaonekana imekwenda kutatua tatizo katika jamii moja kwa moja. Zile za maadhimisho ya Ukimwi, zilinunulia madawa, tunatambua upungufu wa madawa tulionao.
Zile zilizotengwa kwa ajili ya shereje ya uhuru zilipelekwa kwenye upanuzi wa Barabara ya Morocco-Mwenge, wakazi wa Dar ni mashahidi. Barabara ilikuwa na kero kubwa ya foleni, kwa sasa inaelekea kukamilika, kero imepungua kwa kiasi kikubwa.

Ukiachana na hizo, zile zilizotengwa kwa ajili ya sherehe za muungano, akasema ziende zikajenge Barabara ya Air Port Mwanza, hii ndiyo kasi ambayo kila Mtanzania alikuwa anaitaka.
Mimi nikitazama faida na hasara tunazozipata kutokana na staili yake ya uongozi, naziona faida nyingi kuliko hasara.

Nikushauri kwa kuwa umesema mikakati ya upinzani ni kujipanga na uchaguzi ujao ni vyema mkaanza kujipanga,
mkamuacha Magufuli amalize muda wake nina hakika hadi atakapoondoka madarakani, watumishi watakuwa wamenyooka na utakuwa ni mwanzo mzuri wa kutengeneza mfumo wa viongozi kufanya kazi kwa weledi na uadilifu. Mimi ni ndugu yako;
Erick Evarist

Leave a Comment