×

Waliovuna Mishahara ya Watumishi Hewa Wawajibishwe

Magufuli amalizia Baraza la Mawaziri-001Rais Dk. John Pombe Magufuli Machi 15, mwaka huu alitoa amri kwa wakuu wa mikoa nchi nzima kuhakiki watumishi hewa katika taasisi za umma na idara za serikali katika mikoa yao.

Amri hiyo aliitoa wakati anawaapisha wakuu hao wa mikoa na hakika walilifanyia kazi agizo hilo na wamefanya kazi nzuri na wamebaini kuwepo wafanyakazi hewa 2,300 huku Mikoa ya Arusha, Mwanza, Singida, Katavi, Kigoma, Dodoma, Tanga, Geita na Morogoro ikiongoza kuwa na idadi kuwa ya wafanyakazi hewa.

Baada ya kubainika wizi huo wa kutisha hivi sasa Watanzania wanataka kujua wezi hao watachukuliwa hatua gani, au je, watalazimishwa kurudisha fedha hizo za umma?
Imeelezwa kwamba kuna watendaji ndani ya taasisi hizo walitengeneza majina hewa makusudi wakawa wanajilipa na kusababishia serikali hasara ya shilingi 3,000,000, 000, kitu ambacho ni kibaya sana.
Ni dhahiri kwamba mchezo huo mchafu unahusisha watu wengi hivyo mgawo wa fedha hizo ni mkubwa mno na naamini uchunguzi wake ni rahisi kuwabaini.

Ni imani ya Watanzania kwamba kutokana na utendaji makini wa serikali ya awamu ya tano ya Rais Magufuli, utachukua haraka hatua za kisheria dhidi ya walionufaika na fedha hizo za watumishi hewa.

Wizi huu ni wa kimtandao, hivyo ushauri wangu ni vema serikali ikaanza na kufumua mtandao huu hatari kuanzia ngazi za wizara, hazina hadi huko mikoani ambako wizi huu ulikuwa ukifanyika bila woga.
Nasema hivyo kwa sababu, kama serikali itaamua kuwachukulia hatua watu wa chini na kuwaacha vigogo (kama wapo), litakuwa kosa kubwa na ni wazi wizi wa aina hii hautaisha nchini.

Ni vema serikali ikatumia vyombo vyake vya uchunguzi kufuatilia mtandao huu hatari wa wizi wa mishahara hewa na watakaobainika wawekwe hadharani kabla ya kufikishwa katika vyombo vya sheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Watanzania wengi wanajiuliza, ina maana viongozi walikuwa hawalijui hili hadi Rais Magufuli alipoingilia kati? Ukitafakari kwa makini utagundua kwamba wizi huu wa mishahara hewa ni ‘dili’ ambalo linahusisha wengi.

Hakika ukitafakari kwa makini utagundua kuwa kuna baadhi ya viongozi wamepewa dhamana ya kututumikia lakini jukumu hilo wameliweka kando na badala yake wanajilimbikizia mali za umma bila huruma licha ya rais wetu kuonesha njia na kujali zaidi watu anaowaongoza.

Naamini, serikali ikiwaadabisha wote wanaofuja fedha za umma, itawafanya wezi kuogopa hivyo kuokoa fedha za walipa kodi ambao wengi wao ni maskini.

Mungu Mbariki Rais Magufuli, Mungu Ibariki Tanzania.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

1 Comment

Leave a Comment