Mungu ni mwema sana, ikawa mchana ikawa usiku. Imefika Jumamosi nyingine. Tunakutana kwenye uwanja wetu wa kupeana darasa huru la masuala ya uhusiano. Wiki hii tunaijadili mada yenye kichwa cha habari hapo juu, karibu!
Bahati mbaya wanadamu huwa ni wazito sana kuguswa na maumivu ya wenzao. Maumivu ya mtu huwa anayajua yeye mwenyewe. Mtu anapokuwa anamtenda mwenzake huwa si rahisi kujiweka kwenye upande wa yule anayemtenda na haheshimu hisia za mwenzake.
Mwenyewe anajipa
moyo kwa maneno ya kimjini, yale ya; “Kwani tumezaliwa wote? Tumejuana kimjinimjini, tuachane kimjinimjini.”
Anajidanganya kuwa hakuna cha kupoteza. Anachoangalia ni kile kizuri anachokipata kwa wakati huo. Anaongozwa na ushawishi wa fedha, ahadi ya kuolewa, kupewa zawadi kama gari na vitu vingine.
Kwa sababu si mvumilivu, anayatazama maisha ya mchumba wake wa awali, anayaona hayana matumaini. Pengine anaona mateso kila kukicha hivyo ni bora ampate mwingine atakayempa pumziko.
Anasahau kuhusu shida. Apate mwanaume au mwanamke atakayempa fedha za kutosha kama si kumtoa ‘out’, kubadilisha mboga, kuvaa vizuri au kumpa faraja faragha.
Kabla sijaendelea zaidi, ngoja nikupe mfano mmoja. Haya ndiyo maelezo aliyonisimulia rafiki yangu mmoja nilipokutana naye:
“Nilikuwa na mchumba wangu ambaye tulikuwa na mikakati ya kufunga ndoa mwakani. Tumedumu kwenye urafiki kwa takriban miaka mitano. Nilimpenda sana. Niliamini hata yeye ananipenda. Kwa kuwa tayari tulishadumu muda mrefu kwenye uhusiano, tulianza taratibu za kuelekea kwenye ndoa. Tuliwashirikisha baadhi ya ndugu, wakawa wanaelewa mipango yetu.
“Ndugu zangu walikuwa wakimjua na wake walinijua na tulitembeana majumbani mwetu. Yeye alielewana sana na mama yangu. Kila kitu kilikuwa kinakwenda vizuri.
“Kuna wakati alikuwa akija nyumbani. Akishinda kutwa nzima. Ndugu zangu waliamini tunakwenda vizuri na walituombea tuweze kufikia azma yetu.
“Lakini kilichonishangaza, ghafla alianza kubadilika. Alianza kunifanyia visa. Akawa na majibu ya ajabu. Anakasirika katika jambo ambalo hata halihitaji kukasirika. Nilipofuatilia nikagundua anafanya vile kwa sababu kampata mpenzi mwingine.
“Huyo jamaa ameingia kwa gia ya kumuoa mwaka huu. Kwa kuwa mimi nilimuahidi mwakani na jamaa yupo vizuri kifedha, akaona namchelewesha. Huwezi amini nimejaribu kumsihi asiniache. Hajanielewa. Mama yangu amejaribu kuzungumza naye, hataki kusikia lolote. Inaniuma sana maana anakatisha ndoto yangu. Ameshanipotezea muda wangu maana tayari nilishawekeza nguvu kubwa kwake.”
Mfano huo unatupa somo gani? Kama umeshajiridhisha kwamba upo na mwenza sahihi, yakupasa kuwa na msimamo. Haijalishi mwenzako ana hali gani kiuchumi.
Thamini muda. Thamini upendo wake aliouweka kwako. Kama hana kipato, fundishaneni mbinu za kupata kipato. Pambaneni kufikia malengo yenu ya kipato na hata uhusiano. Unapoitenda nafsi ya mtu, kuna uwezekano mkubwa wa wewe kuja kutendwa vilevile baadaye.
Unaweza kumuacha, ukaingia kwenye ndoa na mtu mwingine matokeo yake ukajikuta umeingia kwenye mtu ambaye naye atakuja kukutenda hapo baadaye. Mifano ipo mingi tu. Waswahili wanasema malipo ni hapahapa duniani.
Hakuna mafanikio yanayokuja kirahisi. Kama mmepandana kutoka moyoni, mnapaswa kujaliana kwa kila hali. Tafuteni suluhu ya kila jambo na mtataabika pamoja na hata mkifurahi mtafurahi pamoja!
Tukutane wiki ijayo!