ILIPOISHIA:
Mtu anapofika katika ukingo wa mambo mbalimbali, ndipo Mungu hutokea. Katika hali halisi, madaktari walikuwa wanaomba ruhusu ya kuachana nami. Huu ndiyo wakati nilipofariki kikweli. Bis alikuwa anabubujikwa machozi. DA alikuwa anafanya kila juhudi kumliwaza akimwambia kwamba nilikuwa sijafa na kwamba nikifa angebeba jukumu la kuurudisha mwili Tanzania kwa mazishi.
SASA ENDELEA…
Hivyo, ilikubaliwa kwamba madaktari waache kunipa dawa zaidi na hatimaye kuiondoa mashine na vyombo viliyokuwa vinanifanya niendelee kuishi, kimoja baada ya kingine huku wakifuatilia hali yangu kwa karibu zaidi. Bis na DA walikwenda nyumbani baada ya makubaliano na madaktari kwamba iwapo hali ingefikia mwisho kabisa, wawapigie simu ili warejee hospitali kuushughulikia mwili wangu.
Walipofika nyumbani, baada ya mke wangu kuwaona, aliangua kilio cha juu kwani alikuwa ametegemea kupata habari mbaya. DA akamwambia kwamba nilikuwa bado hai japokuwa nilikuwa mgonjwa sana. Mke wangu hakumwamimi, lakini ndiyo ujumbe waliomfikishia.
Watu wote husika walirejea hospitalini siku iliyofuata, Jumapili ya Agosti 6 walimwacha mke wangu ndani ya gari. Shinikizo lake la damu lilikuwa juu mno kiasi kwamba mfadhaiko mwingine zaidi ungeweza kuleta balaa jingine. Angeweza hata kupata kiharusi.
Bis aliponikuta katika hali ileile, alikwenda nje na kumleta ili anione yeye mwenyewe. Madaktari wakamwambia kwamba nilikuwa nimelala, hivyo sikutakiwa kuamshwa.
Nilibakia katika hali ileile hadi Alhamisi siku ya tarehe 11. Kiukweli, nilikuwa nimeondoka duniani kwa siku nne na nusu. (Mbiguni hakuna mambo ya muda. Mungu alituwekea sisi tu muda katika masuala ya kidunia). Jenerali (Mstaafu) Sam Sarakikya aliyekuwa akifanyiwa uchunguzi wa kimwili mjini London, aliamua kuja Birmingham kuniona.
Alipofika kitandani kwangu, nilifungua macho kwa mara ya kwanza. Nilipomtambua, nilijaribu kumpigia saluti lakini sikuweza kuinua mkono wangu ili uonekane kama nilikuwa napiga saluti; lakini alitambua kilichokuwa mawazoni mwangu, naye akanipigia saluti.
Mungu hufanya kazi yake kimiujiza. Nilipokuwa nimepigwa kiharusi mwaka 2004, Mungu alimpanga Roderick kunitembelea na kukishinda kiharusi hicho kama nilivyosema hapo nyuma. Wakati huu, ujio wa Jenerali Sarakikya ulirudisha uhai wangu. Kwa maneno mengine, Mungu aliutambua upendo na ukarimu wa Jenerali Sarakikya na hivyo kunibariki mimi na yeye.
Wakati nikiwa nimeondoka duniani, kifuatacho ndicho kilichotokea: Kitu cha kwanza kilichotokea ni kwamba fahamu yangu ilirejea. Niliweza kutambua mambo, kufanya uamuzi na kukumbuka kila kitu kwa uwazi kabisa. Nilipokufa, nilijikuta natembea kwenye barabara yenye kokoto ikielekea juu ya mlima.
Akili yangu iliniambia kwamba kwenye kilele cha mlima huo kungekuwa na uzio (fence) na iwapo ningeweza kuuvuka, ningeushinda ugonjwa na mateso niliyokuwa nayo. Ningeibukia upande wa pili nikiwa mtu mwenye afya mpya, nikiwa nimebadilika kabisa. Ningebadilika katika mwonekano na sura, lakini nikiwa katika akili ileile.
Nilijiuliza jinsi ambavyo watu wangenitambua kuwa ni jenerali yuleyule aliyekwenda Uingereza kutibiwa. Nilipata jibu kwamba ingekuwa rahisi iwapo lingekuwa ni jukumu langu kujieleza kwa kuwatambua wao na kuwaeleza kuhusu mambo na mazingira yao.
Nikikutana na mke wangu, ningemweleza mazingira yake ya nyuma, nikawatambua watoto tuliozaa nao na kadhalika. Kisha angekubali kwamba ni mimi tu ambaye nilikuwa na sifa kama hizo na hivyo kukubali kuwa kweli mimi ndiye mumewe. Ningefanya hivyohivyo kwa watu wengine. Hivyo ndivyo ningethibitisha utambulisho wangu.
Hivyo, niliendelea kutembea kupanda mlima huo hadi nilipoufikia uzio. Uzio huo ulikuwa na urefu wa kama mita kumi lakini geti lililokuwa limejengwa kwa mabomba yaliyokuwa yamepakwa madini na seng’enge iliyokuwa na urefu wa mita moja tu. Nikajiambia kwamba ingekuwa rahisi kufika upande wa pili.
Nilipofika sehemu hiyo na kujaribu kupitisha mguu wangu upande wa pili, nilijiona nazidi kuwa na umbo dogo. Nilijaribu kufanya hivyo kwa nguvu lakini kila nilivyojitahidi nikazidi kuwa mdogo zaidi hadi nilipojiona nimekuwa mdogo kama kichwa cha msumari. Mungu hakutaka nifanye upuuzi kwa kupanga kitu ambacho hakikupangwa kufanywa na binadamu. Ukitaka kufanikiwa katika kitu chochote ni lazima kumjumuisha Mungu.
Nikiwa bado nahangaika kujua kulichokuwa kinanitokea, mkono wenye nguvu kubwa ulinikamata na kunipeleka upande mmoja. Mara nilijikuta katika ukumbi mkubwa uliokuwa umemulikwa na taa za aina mbalimbali.
Je, ukumbi huo ulikuwa wa shughuli gani na nini kilijiri kwa Meja Jenerali Mstaafu Msuya? Usikose kufuatilia mkasa huu wa kweli kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko siku ya Jumatano.
SOCIAL MEDIA ZETU:
KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA
INSTAGRAM: @Globalpublishers
TWITTER: @GlobalHabari
FACEBOOK: @GlobalPublishers
SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers
GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz