×

Aboubakar Sadik: Maisha ya Ndoa Yameninyoosha

IMG-20160509-WA0003

Aboubakar Sadik.

Mwandishi: Oscar Ndauka

JINA la Aboubakar Sadik si geni katika tasnia ya habari Bongo. Aboubakar ni Mtangazaji wa Radio One Stereo ya jijini Dar ikirusha matangazo yake sehemu kubwa ya nchi.

Alianza kazi hiyo mwaka 1999 akitokea Kituo cha Redio cha Tanzanite cha jijini Arusha.

Alianza kupata umaarufu kupitia Vipindi vya Dj Show na Nani Zaidi, baadaye umaarufu wake uliongezeka zaidi kufuatia kuwa mmoja wa memba wa Kundi la Kwa Fujo Dj’s ambalo lilikuwa likiwaunganisha baadhi ya ma-Dj kama Francis Siza ‘Majay’ au Majjizo na Kwa Fujo Jr, Dizzo One na Orest Kawau ambao walikuwa wakiporomosha burudani ya disko kwenye kumbi mbalimbali za jijini Dar es Salaam na mikoani.

maxresdefault

Katika mahojiano maalum na gazeti hili mapema wiki hii, Aboubakar alizungumzia maisha yake ya ndoa kumnyoosha kwa maana ya kumtuliza na kumfanya asisikike tena mitaani kama ilivyokuwa zamani. TWENDE NAYE…

Amani: Hebu tuanze na maisha yako ya ndoa, mkeo ni yuleyule uliyefunga naye ndoa mwaka 2003?

Aboubakar: Yeah! Yuleyule, Sarah Mwambungu.

Amani: Mna watoto wangapi sasa?

Aboubakar: Tuna watoto wawili, Assam miaka 12 na Assad miaka mitatu.

Amani: Umewahi kunaswa na mkeo umechepuka au wewe kumnasa yeye amechepuka katika maisha yenu ya ndoa?

Aboubakar: Hata siku moja haijatokea na ndiyo maana tumedumu kwa muda wote huo wa miaka 13.

osz___size__

Amani: Umejifunza nini kwenye maisha ya ndoa na Sarah?

Aboubakar: Nimejifunza jambo kubwa zaidi kuliko ndoa yenyewe ni uvumilivu kwani ndoa ni mtihani mkubwa.

Amani: Umekuwa mtangazaji mtulivu sana kuliko vijana wengine kama wewe ambao kila siku skendo, tukio. Wewe vipi, umedhibitiwa na Sarah au utu uzima?

Aboubakar: Majukumu kaka. Maisha ya ndoa yameninyoosha sana. Kwa hiyo majukumu yanakuwa mengi zaidi kuliko kujiachia kama zamani.

Amani: Vipi kuhusu Kwa Fujo Dj’s, imekufa au ipo hai?

Aboubakar: Ni kundi la kwanza Tanzania lililounganisha redio nyingi kupitia ma-Dj’s wake na kufanya kazi pamoja. Kwenye muungano mafanikio ni makubwa zaidi.

“Kuhusu kufa kwa kundi hilo hapana. Majukumu yalikuwa mengi tukapumzika, ila tuko mbioni kurudi kama zamani. Watu waungane kufanya kazi pamoja mafanikio yanakuwa makubwa kuliko kufanya kazi mwenyewe.”

Amani: Vipi uhusiano wako na Majay?

Aboubakar: Wengi wananiuliza hili swali. Sisi ni marafiki tuliofikia ‘levo’ ya undugu kabisa ni zaidi ya marafiki, tunakutana tunapigiana simu mara kwa mara.

“Tuko katika urafiki kwa miaka 15 sasa hivyo tunajuana vizuri sana kwani tuliwahi kuishi pamoja. Kama hatukupishana wakati huo haiwezi kutokea leo.”

Amani: Kuna madai kwamba anataka kuoa, amekwambia wewe kama rafiki yake mkubwa?

Aboubakar: Hapana sina taarifa hizo labda ni tetesi tu, au kama ni kweli basi mipango bado haijakaa sawa, muafaka ukifika atanijulisha tu.

Amani: Unadhani mwisho wako Radio One ni upi?

Aboubakar: Anayepanga maisha ya mtu ni Mungu, siwezi kujua ya mbele. Ila natamani mwisho wangu uwe mzuri kama nilivyoanza mwanzo, nikumbukwe kwa mazuri niliyoyafanya kwa Radio One nikiwa mmoja wa manguli waliokaa muda mrefu na kufanya mageuzi makubwa hasa kwenye vipindi vya burudani.

Leave a Comment