×

Kubana kwa misuli ya uke (Vaginismus)

vaginismus-in-single-girl

Hali hii wakati mwingine huitwa ‘Vaginism’, ni tatizo linaloathiri uwezo wa mwanamke kuingiliwa ukeni wakati wa kujamiiana, kujisafisha na hata anapochukuliwa vipimo vya ukeni.
Mwanamke anakuwa na tundu la uke kama kawaida na anapata siku zake vizuri lakini unapofika wakati wa kujamiiana basi hiyo njia huwa ngumu kupitika, au hata anapotaka kujisafisha hafiki ndani.

Hali hii inatokana na misuli ya uke kukutana na kubana hiyo njia, endapo utakazana kupenya mwanamke atahisi maumivu makali ya uke. Na hili ni mojawapo ya tatizo la maumivu wakati wa kujamiiana ambalo hutokea wakati wa kuanza tendo.
Misuli inayohusika zaidi na tatizo hili ni aina ya ‘Pubococcygeus’ au kwa kifupi huitwa ‘PC Muscle’. Mwanamke ambaye tayari ana tatizo hili huwa hawezi kujizuia na endapo unaanza kukaribia kumgusa hufumba macho kwa woga na hata kupiga kelele.

CHANZO CHA TATIZO
Vyanzo vya tatizo hili vimegawanyika katika sehemu kuu mbili.
Kwanza ni ‘Primary Vaginismus’. Hii inahusiana na mwanamke kushindwa kabisa kufanya tendo la kujamiiana na wakati mwingine hujihisi hana njia na huwa hana maumivu yoyote na hili huwatokea zaidi wasichana wanaotoka kuvunja ungo au wale wa umri wa kati ya miaka ishirini na ishirini na tano.

Baadhi ya matatizo yanayoweza kusababisha mwanamke kupata tatizo hili ni kama vile; maambukizi ya mara kwa mara ya njia ya mkojo au yutiai inayojirudiarudia kwa wasichana na watoto wa kike, maambukizi ya fangasi ya ukeni mara kwa mara, kudhalilishwa kijinsia kama ubakaji na kumvizia mwanamke na kumwingilia kwa nguvu kabla hajajiandaa, msichana kushuhudia ubakaji wa mwanamke mwingine, au udhalilishaji wa mwanamke mwingine, mtoto wa kike kushuhudia ugomvi wa wazazi nyumbani hasa pale mama anapopigwa na baba au kudhalilishwa, au hata yeye mwenyewe akidhalilishwa na wakubwa wake.
Kuwa na imani kwamba kujamiiana kwa mara ya kwanza ‘usichana’ unapotoka huwa kuna maumivu makali, hii ni imani potofu.

Kuwa na maumivu ya chini ya tumbo au wakati wa kukojoa mara kwa mara, hofu, woga kuhusu tendo la kujamiiana au kuguswa ukeni pia ni mojawapo ya vyanzo vya tatizo.

JINSI TATIZO LINAVYOGAWANYIKA
Tatizo huwa tunaligawanya kufuatana na ukali wa tatizo unaoambatana na maumivu ambayo mwanamke huyapata.
‘First Degree’, hii ni hatua ya kwanza ambapo misuli ya uke hukaza. Hali hii hutulizwa au hutibika kwa kumuondoa hofu mwanamke. Misuli inapokaza njia ya uke hubana na kuachia na ikiruhusu upenyaji huwa hakuna maumivu.

Katika hatua ya pili, misuli hubana na huendelea moja kwa moja bila kuachia na hata ukimtuliza mwanamke wapi bado inabana na huhisi maumivu njia inapojaribu kupenyeka.
Katika hatua ya tatu, misuli huendelea kubana, endapo utajaribu kugusa ukeni hunyanyua hadi makalio juu kutoruhusu kupenya kitu ukeni hata kama anapimwa hospitali huwa vurugu, huendelea hivyo na kubana mapaja.
Katika hatua ya nne, mwanamke hunyanyua makalio, miguu na kukunja miguu hii ni moja ya hatua mbaya za tatizo hili.

Katika hatua ya tano, pamoja na yote ya hatua ya nne, kabla hata ya kuvua nguo kwa ajili ya kupimwa hospitali, mwanamke huanza kutokwa na jasho jingi, moyo kwenda mbio, kutetemeka, kichefuchefu, kutapika na hata kupoteza fahamu mwenyewe bila hata ya kuguswa na kama ndiyo kalazwa katika kitanda cha kupimia akijua kipimo ni cha ukeni huruka na kukimbia au kugombana na wauguzi.
Mwanamke mwenye tatizo hili hakubali hata kidogo kuguswa na mwanaume.

Leave a Comment