×

Vigogo Kutosafiri Nje ya Nchi… Ndege zaruka tupu!

MagufuliiRais Dk. John Pombe Magufuli.

Na Elvan Stambuli, UWAZI
DAR ES SALAAM: Tamko la Rais Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’ la kupiga marufuku safari za nje kwa watumishi wa umma limeelezwa kusababisha baadhi ya ndege zinazosafirisha abiria kutoka nchini kwenda nje kuruka zikiwa na abiria wachache, Uwazi limeambiwa.

Afisa mmoja wa shirika moja la ndege aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutoandikwa jina alisema tangu JPM apige marufuku maofisa wa serikali na mashirika ya umma kwenda nje ya nchi mpaka wawe na vibali maalum pia limesababisha baadhi ya wafanyabiashara kuacha kusafiri, hivyo ndege kuondoka na abiria wachache.

ndegeAlipoulizwa sababu ya ndege kutojaa abiria wakati watumishi wa umma waliokuwa wakisafiri nje ya nchi ni wachache, afisa huyo alisema baadhi ya maofisa waliokuwa wakienda nje walikuwa wakiambatana na wafanyabiashara.

“Wapo wafanyabiashara waliokuwa wakisafiri nje ili kukutana na baadhi ya vigogo ambao ni watumishi wa umma, hivyo sasa safari hizo hawazifanyi.

“Lakini pia wafanyabiashara wengi hawaendi nje ya nchi kutokana na serikali kuminya matumizi ya hovyo  ya fedha zake za kigeni ambayo mengine yalikuwa ni kwa manufaa ya wachache tu,” alisema afisa huyo akisema nchi imeokoa pesa nyingi sana kwa vigogo kutokwenda nje kwa semina na makongamano yao.

maxresdefaultMwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Umma (Chauma), Wakili Hashim Rungwe Spunda.

Ijumaa iliyopita, gazeti hili lilifika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ili kuonana na msemaji au uongozi ili kuusikia kuhusu kuwepo kwa madai hayo, lakini lilijibiwa kuwa, msemaji alikuwa nje ya Dar kikazi na hakukuwa na kiongozi mwenye takwimu hizo.

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Umma (Chauma), Wakili Hashim Rungwe Spunda aliyezungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki alikiri ndege zinazokwenda au kuja nchini miezi ya karibuni kuwa na abiria wachache.

“Ni kweli ndege siku hizi zinakwenda tupu. Mimi nilikuwa Dubai hivi karibuni. Kwenda na kurudi abiria walikuwa wachache sana na nilipowauliza wafanyakazi wa ile ndege husika sababu,  walitaja hizohizo kwamba serikali imebana kila kitu,” alisema Rungwe.
Alisema hivi sasa hata wafanyabiashara hawasafiri kwa ‘kutanua’ kama zamani ambapo mara kwa mara walikuwa wakienda Ulaya, Amerika, China au Arabuni kwa ajili ya manunuzi.

Wakati akipiga marufuku watumishi wa umma kwenda nje ya nchi bila vibali, Rais Magufuli alisema hata baadhi ya bodi za taasisi za umma zilikuwa zikiketi nje ya nchi jambo ambalo lilikuwa linafanya matumizi ya pesa kuwa makubwa pasipokuwa na ulazima.
Mahojiano ya Wakili Rungwe ambayo yamebeba ushauri na maoni yake kuhusu serikali ya awamu ya tano baada ya kuongoza kwa miezi sita tutayatoa katika gazeti hili toleo lijalo.

KUNUNUA NA KUSOMA MAGAZETI YA GLOBAL PUBLISHERS ONLINE, INGIA HAPA==>VODACOM M-PAPER APP

*********

JIUNGE NA SOCIAL MEDIA ZETU:

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

ERIC SHIGONGO INSTAGRAM: @ericshigongo

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz

Leave a Comment