Jana Timu ya Soka ya Global FC inayomilikiwa na Kampuni ya Global Publishers ilishuka dimbani kukipiga na Timu ya Via FC ya Tegeta jijini Dar ambapo Global iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Mchezo huo uliokuwa wa vuta nikuvute ulichezwa kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Tegeta ambapo katika dakika ya 37, mchezaji wa Global FC aliipatia timu yake goli safi baada ya kuwapiga chenga mabeki wa Via walioshindwa kumdhibiti.
Baada ya Global kupata bao hilo, mchezo ulinoga ambapo Timu ya Via ilicharuka kwa kutaka kurudisha bao hilo lakini mpaka timu zinakwenda mapumziko, jitihada zao zilishindwa kuzaa matunda.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote mbili kushambuliana vilivyo lakini katika dakika ya 69, Nyemo Chilongani aliipatia Global bao la pili.
Bao hili liliwafanya wachezaji wa Via kuchanganyikiwa ambapo walionesha kuwa na shauku angalau ya kupata bao moja lakini mpaka dakika 90 zinamalizika, timu hiyo ilikuwa nyuma kwa mabao 2. Kutokana na refa kuongeza muda, Via walijipatia bao la kufutia machozi katika dakika ya 96 hivyo mchezo huo kumalizika kwa matokeo ya 2-1.
Picha na Habari: Hamida Hassan/ GPL

