Ofisa Uvuvi wa Manispaa ya Temeke, Ernest Kamata (kushoto) akiwa na Ofisa Habari wa Manispaa hiyo, Lynn Chawala.
Viongozi hao wakisikiliza maswali yaliyokuwa yakiulizwa na wanahabari (hawapo pichani).
Baadhi ya wanahabari wakichukua matukio katika hafla hiyo.
MANISPAA ya Wilaya ya Temeke imekusudia kutoa elimu juu ya ufugaji wa samaki kwa wananchi kuwaelimisha juu ya ufugaji huo kwa samaki wa maji baridi na maji chumvi kwa kutumia mabwawa majumbani au sehemu zenye maeneo ya kutosha ujenzi wake.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Saalam na Ofisa Uvuvi wa wilaya hiyo, Ernest Kamata, alipokuwa akizungumza na wanahabari ambapo alitaja aina ya samaki wanaoweza kufugwa kwenye maji baridi kuwa ni sato (Nile tilapia) na kambale (African Catfish) ambapo upande wa maji ya chumvi samaki wanaoweza kufugwa ni mwatiko (milk fish), hongwe (African sea catfishes) na tasi (Rabbit fish).
Kamata alifafanua kuwa mfugaji wa samaki anatakiwa kuwa na dhamira ya kweli ya ufugaji, kutokata tamaa pindi aanzapo mradi huo kwani tathmini ya rasilimali ndiyo inamwezesha mfugaji kufanikiwa zoezi zima.
Alisema mfugaji anatakiwa kuzingatia uvumilivu na uthubutu kwa kuelewa kuwa ufugaji wa samaki ni kama ilivyo miradi mingine ambayo mtu anaweza kuwekeza lakini faida yake isiweze kuonekana mara moja.
Kamata alizitaja baadhi ya sehemu ambazo mfugaji wa samaki kwenye mabwawa anaweza kufugia kuwa ni (pond system) vizimba (cages system) na plastic tank system.
Aidha alitaja mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kujenga mabwawa ya samaki ni kuwa na eneo kubwa la kufugia ambalo halina miti mingi, mwinuko wa wastani (1% slope) ili kurahisisha miundombinu ya bwawa kukaa vizuri, udongo wa mfinyanzi ambao haupotezi maji kwa haraka na maji ya kutosha na hewa.
Alitoa rai kwa wananchi ambao wanataka kupata elimu juu ya utaalamu wa ufugaji wa samaki wafike katika ofisi za Halmashauri ya Temeke na watapatiwa elimu juu ya ufugaji bure.
NA DENIS MTIMA/GPL