Said Ally, Dar es Salaam
BAADA ya taarifa kuenea kuwa Klabu ya Mbeya City ipo katika mchakato wa kumtwaa straika wa Azam FC, Mrundi, Didier Kavumbagu, uongozi wa Klabu ya Azam ambayo inammiliki mchezaji huyo umesema kuwa mchezaji mwenyewe ndiye atakuwa na uamuzi wa kuondoka au la.
Mbeya City, imetangaza kukaribia kumnasa Kavumbagu ambaye mkataba wake na Azam umemalizika mwishoni mwa msimu huu, huku akionekana kutokuwa na nafasi kikosini hapo hali inayomfanya kuamua kutafuta njia ya kutokea.
Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba, alisema taarifa za Kavumbagu kutakiwa na Mbeya City wanazisikia tu kwani hakuna mtu aliyemfuata kumtaka mchezaji huyo, lakini akasisitiza kuwa mchezaji mwenyewe ndiye mwenye uamuzi wa mwisho.
“Wachezaji wetu wote wapo likizo mpaka Julai Mosi ambapo kambi yetu itaanza, na siku hiyo kila mchezaji wa Azam atatakiwa kuwasili kambini, tunashangaa kusikia eti Kavumbagu anatakiwa na Mbeya City.
“Lakini kama kweli anatakiwa na hiyo timu ni jukumu lake kuamua aendee au la kwani mkataba wake na sisi umemalizika hivi karibuni,” alisema Kawemba.
