×

Ripoti Kamili; Makaburi Ya Kinondoni Yamejaa

KANUMBA

Na Hashim Aziz

Jua kali la Jiji la Dar es Salaam linaufanya mchana huu kuwa na joto kali, kila anayetembea kwa miguu, anavuja jasho! Natamani kusimama kwenye kivuli lakini napiga moyo konde na kuendelea na safari, mita chache mbele nakutana na kundi kubwa la watu wakivuka barabara, huku wakiwa na nyuso za huzuni.

Baadaye natambua kwamba miongoni mwa watu wale, walikuwepo waliokuwa wamebeba jeneza na walikuwa wakienda kumpumzisha mpendwa wao! Huzuni na majonzi vimetanda eneo hilo, nipo kwenye Makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Nasimama kwa muda kuupisha msafara huo kisha naendelea na safari yangu ambayo inaenda kuishia kwenye geti la kuingilia makaburini hapo, lengo likiwa ni kuonana na uongozi wa makaburi hayo.

Kilichonisukuma kwenda makaburini hapo, mbali na mambo mengine, ilikuwa ni kutaka kujua hali halisi ya upatikanaji wa sehemu za kuzikia na gharama anazotakiwa kuzitoa mfiwa ili ndugu yake azikwe eneo hilo kwani kwa siku za karibuni, kumekuwepo na malalamiko mengi yanayohusu makaburi hayo.

Muda mfupi baadaye, tayari nimeketi mbele ya meza ambayo nyuma yake, yupo mwanaume wa makamo aliyejitambulisha kwa jina la Omary Nassibu ambaye anajitanabaisha kuwa ndiye msimamizi wa makaburi hayo, akiwa anawajibika chini ya Manispaa ya Kinondoni.

Anaonesha ushirikiano mkubwa kwangu na haya ni baadhi ya mambo tuliyozungumza:

UTARATIBU UPI UNATUMIKA UKIHITAJI SEHEMU YA KUZIKA?

“Unapopatwa na msiba na kama unahitaji ndugu yako azikwe hapa, jambo la kwanza ni kufika hapa ofisini kwangu ambapo nitakuelekeza namna ya kuandika barua ya kuomba eneo la kuchimba kaburi. Baada ya kuandika barua na kuiwasilisha hapa, huwa nawasiliana na wenzangu kuangalia kuna sehemu gani bado haijatumika, kama ipo tunakupeleka kisha unaendelea na taratibu zako. Wapo watu ambao huwa wanaomba na huduma ya kuchimbiwa kaburi, hapa kuna vijana ambao hizo ndiyo kazi zao kwa hiyo mnakubaliana na kazi inafanyika kulingana na mlivyokubaliana.

GHARAMA ZA KUPATA ENEO LA KUCHIMBA KABURI ZIKOJE?

“Swali zuri sana, unajua jambo ambalo watu hawalijui ni kwamba hatuchaji kiasi chochote cha pesa ili kupata ardhi ya kuzikia, kama nafasi ipo ni bure kabisa. Isipokuwa, kama unataka uchimbiwe na kaburi, hapo sasa kama nilivyoeleza wewe ndiyo unatakiwa kuzungumza na hawa vijana wanaofanya kazi hapa na kukubaliana nao.

“Wengine huwa wanataka makaburi yakishachimbwa, yajengewe kwa hiyo hizo gharama zinakuwa ni kati ya mfiwa na mafundi lakini sisi kazi yetu inakuwa imeishia hapo.

“Wapo baadhi ya watu wanalalamika kwamba eti wanachajiwa hadi shilingi milioni moja au mbili kupata makaburi, ningependa kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu hili. Kuna baadhi ya watu wakifika hapa, wanataka makaburi ya ndugu zao yawe ya kifahari, mtu anataka kuanzia ndani kuwekwe marumaru, juu kuwekwe mapambo ya ‘marble’ na nakshi nyinginezo.

“Ni kweli ukipiga mahesabu ya vifaa vyote vinavyotakiwa mpaka kaburi la namna hiyo likamilike, linaweza kugharimu mamilioni ya fedha lakini hayo yanakuwa ni matakwa ya mfiwa wala sisi hatuhusiki kwa chochote.

NAFASI ZA KUZIKIA BADO ZIPO?

“Kiukweli, makaburi mengi ya mijini, yakiwemo haya ya Kinondoni yamejaa ila tunachofanya inakuwa ni kutanua kidogo mipaka. Kwa mfano hapa Kinondoni, sehemu zilizobaki za kuzika watu ni chache mno na muda mfupi baadaye tutakuwa hatuziki tena hapa. Watu wanaokuja hapa, wengi huwa tunawashauri kwenda kwenye makaburi yetu mengine yaliyopo Tegeta Kondo, nje kidogo ya mji.

“Hata hivyo, watu wengi huwa wanang’ang’ania kuzika hapa na kutupa kazi ya ziada kuwaelekeza. Napenda pia kutumia fursa hii kuwataarifu watu kwamba wasiwe wakaidi wanapoelekezwa kwenda kuzika kwenye makaburi ya Tegeta kwa sababu hapa pamejaa.

MILA ZA KUSAFIRISHA MAITI UNAZIZUNGUMZIAJE?

“Unajua kuna makabila mengine yana mila zao kwamba mtu akifa lazima asafirishwe kwenda kuzikwa kijijini kwao kama Wachaga. Hawa wanasaidia sana kupunguza msongamano kwenye makaburi ya hapa mjini kwa sababu tukisema kila mkazi wa Kinondoni azikwe hapa, hakuna eneo linaloweza kutosha kwa hiyo naona ni mila nzuri na wengine waige.

VIPI KUHUSU ULINZI MAKABURINI?

“Makaburi yetu hapa yana ulinzi wa kutosha kwa sababu kuna watu wameajiriwa na manispaa kwa ajili ya kufanya usafi nyakati za mchana lakini pia kulinda nyakati za usiku na wanalipwa mshahara kwa ajili ya kazi hiyo.

KUHUSU WATU WANAOZIKWA NA MANISPAA

“Hilo ni swali la msingi sana ambalo waandishi wengi wakija hapa huwa hawaliulizi badala yake wanakazania kuwa tunawatoza watu fedha nyingi kupata makaburi. Nina mambo mengi ya kuieleza jamii kuhusu dhana potofu iliyojengeka mitaani kuhusu tunavyoishughulikia miili ya watu waliokosa ndugu wa kuwazika na kulazimika kuzikwa na manispaa.

“Hata hivyo, kutokana na unyeti wa suala lenyewe, nakushauri uandike kwanza barua kwenda kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, yeye ndiye anayeweza kulifafanua hili,” alihitimisha Nassibu.

KUTOKA KWA MHARIRI

Tayari taratibu za kuwasiliana na manispaa zimekamilika na ripoti kamili ya watu wanaozikwa na manispaa imeshakamilika. Endelea kufuatilia magazeti ya Global Publishers ili kujua undani wa suala hilo.

Leave a Comment