Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini, Gilay Shamika (kulia) akisoma taarifa kwa wanahabari. Pembeni mwake ni baadhi ya viongozi wenzake wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini.
Mkutano ukiendelea.
Wanahabari wakichukua tukio hilo.
WAKALA wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (Tanzania Minerals Audity Agency-TMAA) imejisifia namna ilivyofanikiwa kudhibiti shughuli za uchimbaji na biashara ya madini nchini kwa kujipatia mapato stahiki kupitia usimamizi mzuri na ukaguzi makini hasa kwa kuzingatia uhifadhi na utunzaji thabiti wa mazingira katika maeneo ya migodi.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Gilay Shamika, alisema mbali na kujipatia mapato stahiki kutoka kwenye uzalishaji pia wakala umeweka wakaguzi maalum katika mgodi ya Williamson Diamond uliopo Mwadui, Shinyanga, unaozalisha madini ya almasi na TanzaniteOne uliopo Mererani, Manyara, unaozalisha madini ya Tanzanite.
Alifafanua kuwa katika kipindi cha Julai 2015 hadi Machi 2016, kiasi cha karati 119, 218 za almasi zenye thamani ya Dola za Marekani 56,709,683.28 ziliuzwa na kulipiwa mrabaha wa dola za Marekani 2,774,085.78.
Aliongeza kwamba mbali ya kudhibiti eneo la uzalishaji, wakala pia kwa kushirikiana na jeshi la polisi, TRA, TAA, Idara ya Madini na Usalama wa Taifa umeweka wakaguzi katika viwanja vya ndege na mipaka ili kudhibiti biashara haramu na utoroshaji wa madini nchini.
Alifafanua pia kwamba ukaguzi uliofanywa na TMAA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania uliwezesha baadhi ya kampuni za uchimbaji kuanza kulipa kodi ya mapato na kipindi cha mwaka 2009 hadi Machi 2016, kampuni mbalimbali zililipa jumla ya Shilingi bilioni 732.6 kama kodi ya mapato.
NA DENIS MTIMA/GPL


