×

Waliobomolewa Maswa walia na wizi, DC aja juu

kamandashinyanga2Na Mwandishi Wetu

WANANCHI wa Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu wamelia wengine kwa kwikwi baada ya kubomolewa nyumba zao hivi karibuni huku wakilalamikia wizi waliofanyiwa wakati wa ubomoaji.

Wakizungumza na gazeti hili wananchi hao wa vijiji vya Mwabayanda na Kinamwigulu walilalamikia ubomoaji wa nyumba zao 19 wakidai kuwa ulifanywa kimakosa na kusababisha kero kubwa kwao.

Habari zinasema ubomoaji huo ulifanywa na Kampumi ya Subira General Supplies ya mjini Shinyanga chini ya ulinzi wa askari polisi huku wenye nyumba wakiwa hawapo.

“Wengi tulikuwa kwenye shughuli zetu na walipoulizwa na mashuhuda walisema walikuwa wakitekeleza amri ya mahakama,” alisema Madaha Milinga mmoja wa waathirika hao.

Akaongeza kuwa baadhi ya nyumba zilivunjwa usiku na mali zao kuibwa kitendo ambacho hawawezi kukivumilia.

Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki (CCM) alikiri kutokea kwa tukio hilo na akasema mbele ya wananchi hao kuwa hapingani na utekelezaji wa amri hiyo ambayo ni ya kisheria lakini utaratibu uliotumika kuvunja nyumba hizo bila kuwepo wenye nyumba na viongozi wa maeneo husika ni ukiukwaji wa sheria za nchi.

“Ninachokilalamikia ni jinsi ubomoaji ulivyofanyika, wabomoaji hawakufuata utaratibu kwani zipo nyumba zilibomolewa usiku na nyingine wakati wenye nyumba wakiwa makanisani, mbaya zaidi wameshindwa kuwajulisha watendaji wa vijiji au wa kata,” alisema Mbunge Ndaki.

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya (DC) Maswa, Rosemary Kirigini (pichani) alikiri kufahamu tukio hilo na akasisitiza kuwa lazima sheria ifuatwe.

“Nashauri, kama kuna watu walipigwa na kuibiwa mali zao wakati wa utekelezaji wa amri hiyo, wananchi kama wana ushahidi, watafute haki zao kwenye vyombo vya sheria,” alisema.

Leave a Comment