×

Laana ya baba ‘Yammaliza’ Diamond!

Diamond-PlatnumzStori: Mwandishi Wetu, Ijumaa

Dar es Salaam: Waswahili wanasema, endapo mtoto atamfanyia mzazi wake jambo la kumuumiza, hata kama mzazi hatasema; ‘nakulaani mwanangu’, ile kusononeka tu, inaweza kuwa laana na hicho ndicho kinachodaiwa kummaliza Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Wakizungumzia tukio la Diamond kukosa Tuzo za The Black Entertainment Television (BET) zilizotolewa wikiendi iliyopita nchini Marekani, baadhi ya wadau wa muziki walisema kulikuwa na mazingira mazuri ya msanii huyo kung’ara kama ilivyo kawaida yake lakini kutokana na kuendelea kumuwekea ngumu baba yake, mzee Abdul Juma, mambo yake lazima yatambumia.

baba diamond (2)Walisema siku chache baada ya Diamond kukwea pipa kwenda Marekani kushiriki utoaji wa tuzo hizo, huku nyuma baba yake huyo alizidiwa na kukimbizwa hospitalini lakini cha kusikitisha alikosa fedha za matibabu, wakati mwanaye ana uwezo mkubwa kifedha akitajwa kuwa na utajiri wa zaidi ya Sh. bilioni 8.

“Jamani tuende mbele na kurudi nyuma, Diamond laana ya baba yake inammaliza, kitendo cha kuendelea kumkaushia na kumuacha aendelee kuteseka hakiwezi kuwa na baraka kwenye maisha yake.

“Kwenye tuzo zile kila mtu hasa Team Diamond waliamini angeshinda lakini amekosa, ukifuatilia sana watu wanaojua maisha watakuambia ile kunung’unika kwa baba yake inaweza kuwa sumu kwa sababu kama mtakumbuka siku Diamond anaondoka kwenda Marekani kwenye Tuzo za BET, ndiyo siku ambayo baba Diamond alizidiwa na kukimbizwa hospitalini lakini akakosa fedha za matibabu.

diamondplatnumz

“Hivi kwa nini hataki kumsamehe kiroho safi na akayaacha maisha yaendelee?” alihoji Rashid Idd ‘Chid Boy’ wa Kariakoo, Dar.

YAMEWAKUTA WENGI

Ikazidi kuelezwa kwamba, historia inaonesha kuwa, watoto ambao hawakuwa na maelewano mazuri na wazazi wao, mwisho wao ulikuwa mbaya.

“Siyo kwa kulaaniwa waziwazi, hapana! Mzazi anaweza akashindwa kukulaani kwa kuwa ni mwanaye na hapendi kukuona unaharibikiwa lakini atakapokuwa ananung’unika kwa wewe kushindwa kumsaidia wakati uwezo unao, sononeko lake haliwezi kupita hivihivi.

“Hiki ndicho kinachompata Diamond, anaweza akachukulia poa kwa kuwa mambo yake mengine yanamnyookea lakini asipofanya uamuzi sahihi sasa hivi, kuna siku yatamkuta mazito na atajuta.

“Yule mzee Abdul wala hahitaji mambo makubwa ya kumfanyia, kama alimkosea huko nyuma, asahau tu! Amsaidie kwenye masuala ya matibabu, fedha ya kula isimpige chenga ili na yeye aonekane ni baba wa staa mkubwa ndani na nje ya Bongo.

“Hivi kweli mwanao ana mafanikio makubwa halafu uende hospitalini ukose fedha ya matibabu, utibiwe kwa msaada! Hizi laana nyingine huwa tunazitafuta wenyewe,” alisema mmoja wa wazee ambao ni watu wa karibu wa baba Diamond.

NI TATIZO LA MUDA MREFU

Kwa muda mrefu baba Diamond amekuwa akiishi maisha ya kuungaunga huku mwanaye ‘akitumbua fedha’ ambapo hivi karibuni daktari mmoja alisema kuwa, kwa kinachoendelea kati ya wanafamilia hao, Diamond anamuua baba yake bila kujua.

“Msongo wa mawazo ni tatizo kubwa duniani linalotokana na kusheheni kwa mawazo ya kila wakati, husasan kuhusu maisha au afya. Kwa hiyo anachofanya Diamond kwa baba yake ni sawa na kumuua kwa sababu ya kumsababishia msongo,” ndivyo alivyosema daktari Rweyemamu wa hospitali moja ya jijini Dar na kuongeza:

“Nimekuwa nikisoma habari mbalimbali kwenye Magazeti Pendwa lakini hili la Diamond kumtelekeza baba yake mimi naona lina mapana yake. Najua utetezi wa Diamond ni kwamba, baba alimtelekeza mama yake (Sanura Kassim) yeye akiwa mtoto.

“Kwa hiyo malezi yote, ameyapata kwa mama hadi kufika kwenye kiwango cha mafanikio. Lakini pia nimewahi kusoma kwamba, baba aliomba msamaha yaishe, atambulike kama baba lakini mtoto akagoma.

“Kuna wakati nikasoma kwamba, yule mzee anasumbuliwa na miguu, mara sijui ugonjwa wa kansa ya ngozi. Pia amekuwa mtu wa kuumwa mara kwa mara.

“Yule mzee atakuwa na magonjwa mengi, hasa yanayotokana na msongo wa mawazo. Mawazo yake kwa sasa ni kitendo cha kuona mafanikio ya mwanaye akilinganisha na maisha yake magumu bila msaada.

“Binadamu yeyote, anapomwona mtu wake wa karibu amefanikiwa na yeye hali duni huku huyo aliyefanikiwa anaweza kumsaidia akaondokana na hali duni, lazima asumbuliwe na msongo.”

BABA DIAMOND ANASEMAJE?

Ijumaa lilimpigia simu baba Diamond kuzungumzia juu ya mwanaye kukosa tuzo lakini pia kunena chochote kuhusiana na kile kinachoongelewa na watu kuwa manung’uniko yake yanamfanya Diamond aanze kukwama kwenye mambo yake.

Hata hivyo, kuonesha kuwa hataki kumzungumzia mwanaye huyo, alimsikiliza mwandishi wetu kwa umakini lakini hakusema chochote zaidi ya kukata simu. Hata alipotumiwa sms hakujibu.

DIAMOND NAYE

Yeye hakupatikana mara moja kwa kuwa wakati gazeti linakwenda mitamboni alikuwa bado yuko Marekani lakini kuhusu kukosa Tuzo ya BET alinukuliwa na mtandao mmoja wa burudani akisema:

“Kila kitu kimeenda fresh na tuzo kwa upande wa Afrika imeenda kwa Black Coffee, unatakiwa umshukuru Mungu kwa kila kinachotokea na hata ukiangalia kwa mwaka jana, Tanzania ndiyo nchi ambayo imepokea tuzo nyingi sana za International kwa hiyo watu waendelee tu kusapoti.”

Leave a Comment