×

Ziara ya Benjamin Netanyahu na Kuvamiwa kwa Entebbe

netanyahu-and-museveniWaziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyau akiwa na mwenyeji wake rais wa Uganda, Yoweri Museven mara baada ya kuwasili uwanja wa kimataifa wa ndege wa Entebbe, Uganda.

Na Leonard Msigwa

ILIKUWA asubuhi tulivu baada ya usiku ambao kamwe hautosahaulika kwa wananchi wengi wa Uganda wakiongozwa na dikteta Idd Amin. Kama wananchi wengine wa mjini Entebbe kijana  Chriss Luvunia  alikuwa amelala pembezoni mwa ufukwe wa Ziwa Victoria kilomita 40 kutoka mji mkuu wa Uganda, Kampala. Akiwa amelala alisikia milio ya risasi na milipuko iliyofanya anga kutawaliwa na mwanga na miale inayotokana na mapigano hayo.

Kwenye makazi yake alikuwa akiishi na vijana wengine watatu ambao wote walikuwa waajiriwa wa jeshi la Uganda kitengo cha usalama barabarani. Wakati huo akiwa na umri wa miaka 26 aliona vyema kilichokuwa kikiendelea uwanja wa kimataifa wa ndege wa Entebbe.

idd amin dadaaRais wa zamani wa Uganda, Idd Amin.

Na wakati haya yote yakitokea alikuwa na miezi michache toka arejee nchini Uganda akitokea jijini Dar es Saalam kwenye mafunzo maalum ya kazi. Na tukio lake la kwanza kushuhudia ni milio ya risasi na milipuko ikionekana kama jaribio la kimapinduzi dhidi ya serikali ya Amin.

 “Tuliwaona wanajeshi wakitembea kutoka uelekeo wa uwanja wa ndege, wakiwa na silaha huku wakionekana kuwa na tahadhari kubwa,”  alisema  Luvunia, ambaye kwa sasa amestaafu.

“Tulihisi na kuamini kuwa serikali yetu imeangushwa na kuna jambo baya linaendelea uwanja wa ndege,” alisisitiza.

Baada ya vurumai ile ya usiku wakazi wengi wakiwa wamejifungia ndani ya nyumba zao wakiwa na woga na hofu kubwa Luvunia alielekea kazini kwake ndani ya uwanja wa ndege ambako muda mfupi uliopita kuna tukio kubwa lilikuwa limetokea.

Eneo lote lilikuwa kama jangwa huku wanajeshi wanaowajibika kulinda mali kila mmoja akiwa amepigwa na butwaa.

Kama kawaida ya polisi, Luvunia na wenzake walianza ukaguzi  katikauwanja wa ndege hususani sehemu ya njia ya ndege. Huko waliona mabaki ya risasi na vitu vingine vinavyoweza kusababisha ajali ya ndege, hivyo waliviondoa na kusafisha eneo hilo.

Baadaye ikaja kugundulika kwamba yale mapigano na milipuko ya usiku ilikuwa ni operesheni ya kikosi maalum cha jeshi la Israel kuwakomboa raia 104 waliokuwa wanashikiliwa na vikosi vya Amin kwenye jengo la kujazia mafuta ya ndege.

Uvamizi wa Entebbe umeandikwa sana kwenye vitabu, makala, vipeperushi na kutengenezewa sinema. Shujaa wa Israel alikuwa komando Sayaret Matkal wa kikosi maalum pia kuuwawa kwa kiongozi wa operesheni hiyo, Yonatan Netanyahu, ni vitu ambavyo kamwe havitasahulika katika uvamizi wa Entebbe.

Jambo la kushangaza miaka 40 baada ya operesheni hiyo mdogo wake  Netanyahu ambaye kwa sasa ni Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyau,  ameitembelea Uganda na amefika hadi Entebbe mahali ambako kaka yake alipigwa risasi na kufariki. Ziara yake ni ya kwanza kwa kiongozi wa juu kutoka Israel kuitembelea Uganda tangu uvamizi wa Julai mwaka 1976.

Madhara ambayo hayatasahulika

Wengi wa walioshiriki operesheni hii tayari wameshafariki, maandiko mengi yameandika kuhusu Dora Bloch, raia aliyekuwa na uraia wa nchi mbili za Uingereza na Israeli ambaye alikombolewa kutoka hospitali alikokuwa amelazwa na kuuwawa dakika chache baada ya kuachwa na ndege.

Muda mchache baada ya uvamizi huo vikosi vitiifu vya Idd Amin vilifanya msako maalumu wa kuwakamata wote waliohusika na uvamizi huo. Walimkamata Fabian Rwengyembe, aliyekuwa muajiriwa wa idara ya usafiri wa majini kwenye Ziwa Victoria. Pia walimkamata msaidizi wake Lawrence Mawanda, na Mohammed Muhindo aliyekuwa kitengo cha uthibiti usafiri wa anga usiku wa tukio.

Baada ya kuwakamata waliuawa.  Ndugu wa Mawanda walisema ndugu yao aliuawa na kukutwa amepigiliwa misumari  iliyozama kichwani.  Inasemekana wote watatu walikufa kifo cha mateso cha aina moja.

Wycliffe Kato, aliyekuwa msaidizi wa mamlaka ya usafiri wa anga alikamatwa miezi miwili baadaye na kuteswa lakini alifanikiwa kutoroka na kwenda kujificha nje ya nchi. Bila kuwa na ushahidi wa wazi, lakini ni ukweli usiopingika kwamba mauaji na mateso hayo yalikuwa ni amri ya Idd Amin mwenyewe.

Sababu za kufanikiwa kwa uvamizi huo

Siku chache kabla ya uvamizi,  Meja Were aliyekuwa mkuu wa shirika jipya la usafiri wa anga nchini Uganda alitoa amri ndege ya abiria isiondoke kwenye uwanja wa ndege wa zamani wa Entebbe ambako mateka wa Israel walikuwa na hivyo kuhamishiwa jengo jipya la abiria uwanjani  hapo.

“Vikosi vya Amin vilikuwa na wasiwasi mkubwa kuwa vikosi vya Israel vingevamia na kuwaokoa mateka wote kutokana na historia yao kama walivyofanya, hivyo walimjuza dikteta Amin kila kitu,” alisema mwanajeshi mstaafu ambaye hakutaka jina lake liwekwe wazi.

Pamoja na yote yaliyotokea, Amin alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha raia wote wa Israel wanakuwa salama na wanalindwa na kutafutwe njia mbadala na salama kumaliza tatizo hilo.

Kwa mfano wakati akiwalazimisha Israel kuwaachia wafungwa mbalimbali kutokana na tuhuma za ugaidi, yeye mwenyewe alienda kuzungumza na mateka hao mara kadhaa, na walitimiziwa baadhi ya mahitaji yao kama ilivyokuwa kwa Ilan Hartuv, mtoto wa kiume wa Dora Bloch aliyeruhusiwa kwenda hospitali kuzungumza na daktari anayemtibu mama yake kwenye hospitali ya Mulago.

Ubabe wa Israel

Ilikuwa ni tukio la kuonyeshana ubabe baina ya Israel na Amin kwa msingi kwamba watu wote wanaotafuta amani huwa wanajiandaa kwa vita. Hivyo ndivyo Waisraeli walivyofanya kwa kutumia muda mwingi kufanya mazungumzo na serikali ya Amin huku kimyakimya wakijiandaa kuivamia Entebbe. Ni kama vile Amin alikuwa anafanya mazungumzo ya pekee yake.

“Mtu yeyote aliyejaribu kupiga simu kwenye kituo cha uthibiti mawasiliano ya ndege kwenye uwanja wa Entebbe siku chache kabla ya uvamizi simu zote zilikuwa zinajibiwa na sauti kutoka Jerusalem, mji mkuu wa Israeli,” alisema  Luvunia.

Hii inaweza kuwa lilikuwa onyo kubwa kwa serikali ya Amin, kama ilivyodhibitishwa kutoka mwaka 1973  kwenye vita ya Yom Kippur kwamba Waisraeli wana vifaa maalumu vya kuiba mawasiliano na kuhamishia kwao na walivipenyeza na kuviweka Entebbe,  hali iliyokuwa rahisi kwao kuteka mawasiliano toka mi huo.

Ukweli ni kwamba, marubani wa shirika la ndege Uganda waligundua vitu mbalimbali wakati wakiendesha ndege ambapo walitambua fika watu wa kuongoza rada hawakuwa na utaalamu sahihi ndiyo maana walishindwa kugundua kuingiliwa kwa mawasiliano yao na watu wa Israel. Walikuwa hawana tofauti yoyote na raia wa kawaida wasio na mafunzo yoyote.

Mbali na suala hilo pia hakukuwa na mawasiliano mazuri kati ya wananchi na waongoza rada, hili lilikuwa kosa kubwa zaidi lililopelekea kuwavimiwa kwa Entebbe.

Mashirika ya ndege ya kigeni

Kitabu kilichoandikwa na Steven Carol kinachoitwa “From Jerusalem to the Lion of Judah and Beyond”,  kuhusu sera za Israel kwenye nchi za Afrika,  kinaeleza bayana kuwa Julai 2, jasusi toka nchini Israel alisafiri kutoka London hadi Nairobi, akakodi ndege na kupaa katika anga la uwanja wa Entebbe kisha akapiga picha za uwanja wa zamani. Aliporejea Nairobi alizituma picha zile Israel.

Ilitakiwa kuifuatilia na kuilazimisha kutua chini kisha ikaguliwe , wanajeshi wakiupelezi walitakiwa kuchukua hatua hizi mapema zaidi. Wangefanya hivyo ingesaidia kujilinda na kuzuia uvamizi huu ambao ulimtia aibu Amin na vikosi vyote vya ulinzi.

Miaka mingi imepita

Ugomvi ambao Amin alijaribu kuuingilia kati ya Israel na Palestina bado upo wakati huu Israel akiwa mbabe na anayeogopwa. Ugomvi unaendelea kutokana na matukio ya 1973 na 1976 lakini ukweli ni kwamba dunia nayo imebadilika.

Idi Amin amepumzika kwenye makazi yake ya kudumu nchini Saudi Arabia alikokimbilia baada ya kupinduliwa na majeshi ya Tanzania.

Waziri Mkuu Yitzhak Rabin, aliyesimamia na kuamuru uvamizi wa Entebbe alishatangulia mbele za haki baada ya kuuwawa na mlinzi wake wa karibu.

Ujio wa Benjamin Netanyahu umeweka wazi mengi yaliyokuwa yamejificha kuhusu kuvamiwa kwa Entebbe, na Rais Museveni amepongeza uamuzi huo kutokana na ukweli Amin alikuwa mbishi na mtu asiyependa kusahaulika.

Mwisho uvamizi wa Entebbe mwezi Julai 1976 ulithibitisha kwamba Uganda, Jumuiya ya Afrika Mashariki kamwe haziwezi kulingana katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia na maendeleo kwa ujumla.

Leave a Comment