Waziri Mkuu wa zamani wa Italia, Silvio Berlusconi.
Leonard Msigwa na Mtandao
WAZIRI MKUU wa zamani wa Italia, Silvio Berlusconi ameruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo. Anaonekana kunyong’onyea na amepungua sana lakini ameonya kwamba haimaanishi huo ndio mwisho wake kwenye duru za siasa.
“Nahitaji kupumzika kwa muda wa miezi miwili kisha nitarejea kuwatumikia Waitaliano” alisema Bw. Berlusconi mwenye umri wa miaka 79 alipozungumza na vyombo vya habari na wananchi wanaomtakia heri nje ya Hospitali ya San Raffaele jijini Milan.
Waziri Mkuu huyo mstaafu na mmiliki wa Klabu ya Soka ya Ac Milan ataendelea kujiuguza katika makazi yake yaliyopo Arcore, karibu na Jiji la Milan, Kusini mwa Italia chini ya uangalizi wa madaktari kutoka San Raffaele.
“Upasuaji wa moyo aliyofanyiwa Berlusconi ulikamilika kwa ufanisi chini ya madaktari bingwa wa moyo kutoka hospitali hiyo ndani ya saa mbili ikiwa ni kwa ajili ya kuondoa mshipa wa aota. Maisha ya Berlusconi yamekuwa hatarini kwa sasa na yeye anatambua hilo” Daktari wake Alberto Zangrillo alisema.
Berlusconi aliyetikisa katika siasa za Italia kwa miongo miwili amewekewa mshipa wa plastiki utakaodumu kwa muda wa miaka 15 hadi 20 na atahitajika kufanyiwa tena upasuaji baada ya muda huo.