Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.
Na Leonard Msigwa
“MIMI nang’atuka, lakini ninaendelea kuamini kuwa bila CCM madhubuti, nchi yetu itayumba,’’ alisema Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wakati akikabidhi uenyekiti wa CCM taifa, kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (wakati huo) Ali Hassan Mwinyi, mwaka 1990.

Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa mwenyekiti wa taifa wa CCM kuachia madaraka na kumkabidhi rais aliye madarakani uenyekiti wa chama taifa na utaratibu huo unaendelea mpaka sasa. Rais anayeondoka madarakani ambaye pia anakuwa na cheo cha uenyekiti wa chama taifa humkabidhi rais aliyeingia madarakani endapo ametokea CCM.
Masikio ya Watanzania walio wengi yataelekezwa Dodoma siku ya tarehe 23 Julai 2016. Pale mwenyekiti wa sasa wa CCM Dr. Jakaya Mrisho Kikwete atakapokabidhi uenyekiti huo kwa Dr. John Pombe Magufuli ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.
Mengi yanazungumzwa juu ya hatma ya CCM baada ya mwenyekiti mpya kukabidhiwa madaraka. Ifuatayo ni tathmini ya hatma ya CCM ikiwa chini ya Rais Magufuli.
Tumbua majipu kuendelea
Ni ukweli usiopingika kwamba jasiri haachi asili, majipu yote ndani ya chama tawala hayatakuwa salama chini ya Mwenyekiti Magufuli. Huu ni wakati wa majipu kuanza kujitenga kando kumpisha mwenyekiti mpya.

Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa.
Kuimarika kwa chama
CCM walipatwa na mpasuko mkubwa wakati wa kura za maoni ya nafasi ya urais, chama kiligawanyika na bado vidonda vibichi na vingine vina makovu. Kaulimbiu ya kutumbua majipu imezidisha imani kwa wananchi walio wengi. Ujio wa mwenyekiti mpya umewafanya wataalam wa siasa kuwa na imani kubwa kwa chama kuzidi kuimarika kuliko sasa.
Uwazi na uwajibikaji ndani ya chama
Rais Magufuli anaonekana kuwa mkali ndani ya serikali na hana mchezo kwa wote wanaofanya mambo kimazoea. Nguvu hiyo akiingia nayo ndani ya CCM hakuna kizuizi kitakachozuia suala zima la uwajibikaji ndani ya chama.

Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
Uadilifu wa viongozi
Mwenyekiti huyo mtarajiwa ameshatumbua watu wengi serikalini na bado anatumbua katika kuhakikisha viongozi wanakuwa waadilifu. Hakuna atakayebisha kwamba tumbuatumbua hiyo itaendelea hadi ndani ya chama kuhakikisha viongozi wake wanakuwa waadilifu.
Nguvu ya mwenyekiti kuongezeka
Rais Magufuli anaonekana mtu asiye na utani katika kazi. Siamini hata kidogo yale yaliyovumiliwa na mwenyekiti anayemaliza muda wake kama yatavumiliwa na Rais Magufuli. Masuala kama makundi ndani ya chama, malumbano ya wanachama na kupiga kelele mbele ya mwenyekiti, sitarajii kuyaona tena chini ya mwenyekiti mpya.
Mabadiliko makubwa katika uongozi wa chama
Imekuwa kawaida kwa mwenyekiti mpya kuingia madarakani na safu yake mpya ya uongozi. Mzee Mkapa alipoingia madarakani, katibu mkuu aliyekuwepo, Lawrance Gama, alimpisha Philip Mangula. Alipoingia mwenyekiti anayemaliza muda wake katibu mkuu mzee Mangula alimpisha Yusuph Makamba (akaja William Mkama) na sasa yupo Abdulrahman Omari Kinana. Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanampa nafasi ndogo sana Kinana kuendelea kuwa katibu mkuu kutokana na historia iliyojengeka ndani ya chama.

Abdulrahman Omari Kinana.
Mwisho yatazungumzwa mengi kuhusu ujio wa mwenyekiti mpya wa CCM, lakini ukweli utabaki kwamba “Rais Magufuli amekuwa mtu asiyetabirika katika utendaji wake wa kazi. Ni mtu wa ‘hapa kazi tu’, tusubiri nini kitatokea baada ya Dk. Kikwete kumkabidhi uenyekiti Dk. Magufuli”.
KILA LA KHERI UCHAGUZI MKUU WA CCM TAIFA!
