BAADHI ya wananchi wa Songwe mkoani Mbeya wameeleza kero yao kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala kwamba wanadai mafao yao kwa Mkandarasi Kundan Singh tangu mwaka 2012 bila mafanikio.
Wananchi hao walimwambia mkuu huyo wa mkoa kwamba mkandarasi huyo alikuwa akijenga Uwanja wa Ndege wa Songwe nao kufanya kazi mbalimbali lakini wamekuwa wakidai mafao yao yakiwemo makato ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa zaidi ya miaka minne sasa.
Mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Joshua Mwasilonde alisema yeye na wenzake wamekuwa wakidai mafao yao tangu mwaka 2012 walipomaliza mkataba na mkandarasi huyo.
“Kila tunapofuatilia malipo yetu, tumekuwa tukipigwa kalenda bila sababu za msingi. Hivyo tunakuomba mkuu wa mkoa utusaidie jambo hili kwani tunajua serikali ilishamlipa fedha zake, hivyo anapaswa kutulipa haki yetu ili nasi tuweze kuendesha maisha yetu,” alisema Mwasilonde kwa uchungu.
Akijibu kero hiyo, Makala alisema wamegundua kuwa licha ya mkandarasi huyo kuwakata makato ya NSSF, alikuwa hapeleki makato hayo kwenye mfuko huo kama sheria inavyotaka, hivyo akaamuru ifanyike kila njia akamatwe mara moja ili alipe fedha hizo.
“Kwa kuwa serikali iliingia mkataba na mkandarasi huyo na kumalizana naye bila kuacha deni lolote, wafanyakazi hao wanapaswa kulipwa kwa kuwa walikuwa ni wafanyakazi halali.
“Serikali tulimaliza mkataba na mkandarasi huyo na tayari alishachukua haki zake zote naye lazima atoe haki kwa wananchi hao,” alisema Makala.
Akaongeza: “Atafutwe popote alipo hata kwa nguvu za dola ili aweze kuwatendea haki wananchi waliotumia nguvu zao katika kuhakikisha uwanja wa ndege unajengwa na kukamilika.”
