×

Kazi ya Serikali ya Magufuli imeanza rasmi Julai Mosi

magufulikijanNianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutuweka hai hadi hii leo ninapoandika makala haya, hivyo ahimidiwe milele.

Baada ya kusema hayo niseme kuwa baada ya Bunge la Bajeti kumaliza kazi ya kupitia na kuchambua bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2016/2017 mjini Dodoma hivi karibuni, kazi iliyofanywa na wabunge na kuipitisha, kazi ya serikali ya awamu ya tano ndiyo imeanza rasmi.

Hii ni bajeti ya kwanza ya Serikali ya Rais Dk. John Magufuli ambayo utekelezaji wake umeanza Julai Mosi mwaka huu na ndiyo itakuwa dira ya utekelezaji wa ahadi mbalimbali zilizoahidiwa na kiongozi huyo wa nchi.

Rais Magufuli ameingia madarakani katika nyakati tofauti ukilinganisha na  watangulizi wake wote. Hakuna ubishi kwamba mtangulizi wake, Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete alionja chungu ya kuibuka kwa mitandao ya kijamii ambayo ilikuwa au inasambaza taarifa kwa kasi ya ajabu kwenye jamii.

Kila ahadi ambayo serikali na wabunge wa awamu hii waliyoitoa kwa wananchi imerekodiwa na kuwekwa kwenye kumbukumbu sehemu fulani. Najua katika mwaka wake wa kwanza wa bajeti yake hii, wakati utakapofika wananchi watapima utekelezaji wa baadhi ya mambo ambayo serikali iliahidi kama yametekelezwa au la.

Ndiyo maana nasema kwamba Julai Mosi ndiyo hasa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Magufuli imeanza kazi rasmi japokuwa katika miezi yake ya kwanza tangu ikabidhiwe nchi tumeona serikali inavyotaka mambo yake yaende.

Hakika hatua ambayo serikali hii mpya imechukua ni sawa na mtu aliyehamia katika nyumba mpya ambapo jambo la kwanza huwa ni kufanya usafi na kurekebisha hiki na kile ili kuiboresha.

Ni matarajio yangu kwamba katika mwaka huu wa kwanza serikali itatimiza baadhi ya ahadi zake kwa kiwango cha kuridhisha na kitakachokubalika na hii ni kazi ya mawaziri, manaibu wao, wakuu wa mikoa, wilaya pamoja na wakurugenzi wa wilaya walioteuliwa na mheshimiwa rais hivi karibuni.

Kila mteuliwa atambue kuwa kushindwa kutekeleza ahadi za serikali kwa wananchi ni kuifanya iwe vigumu kuaminika kwamba itatekeleza ahadi nyingine katika bajeti za serikali zinazokuja.

Watanzania wana ndoto nyingi na serikali hii mpya, watataka kuona viwanda vikifufuliwa, wanafunzi hasa wa shule za msingi wakisoma wakiwa wameketi katika madawati na wale wa sekondari, maabara zao zikiwa na vifaa pamoja na kuwa na walimu wa kutosha.

Wananchi wanatarajia kuona huduma za afya zikiwa zimeboreshwa, ndege mali ya taifa zikifanya kazi, ujenzi wa reli za kiwango cha kisasa na maboresho katika bandari za Mtwara, Lindi, Dar na Tanga zikiwa zimeboreshwa.

Niwapongeze wote walioteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali na wajuwe kwamba ndoto za Watanzania za maendeleo zipo migongoni mwao, atakayezembea, hatavumiliwa.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave a Comment