×

Ukweli Kuhusu Maiti Zinazozikwa na Manispaa

makaburiNa Hashim Aziz

Yapo madai mbalimbali kwamba maiti zinazokosa ndugu na kulazimika kuzikwa na manispaa, huwa hazipewi heshima inayostahili, ikiwa ni pamoja na maiti zaidi ya moja kuzikwa kwenye kaburi moja, baadhi kukatwa viungo na nyingine kufukiwa kama inavyofukiwa mizoga ya wanyama.

Kufuatia madai hayo ambayo yapo kwenye jamii kwa muda mrefu, gazeti hili liliamua kuanza uchunguzi wa kina kubaini kama yana ukweli wowote, na kama ni kweli, ni nani hasa anayehusika na unyama huo?

MAKABURI YA KINONDONI

Uchunguzi unaanzia kwenye Makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo gazeti hili linakutana ana kwa ana na msimamizi wa makaburi hayo, ambaye pia hushiriki kwenye zoezi la kuzika maiti za namna hiyo, Omary Nassibu.

Mbali na mambo mengine, msimamizi huyo anamueleza mwandishi wa ripoti hii kusikitishwa na madai hayo ambayo naye anakiri kuwahi kuyasikia lakini anasita kutoa ufafanuzi wa kina kwa sababu yeye si msemaji wa serikali.

“Nakushauri uende ukaonane na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni au Mkurugenzi wa Jiji, akikupa ruhusa ya maandishi, ndipo nitakapokuwa tayari kukufafanulia kwa kina kuhusu madai hayo na Watanzania wote wataujua ukweli,” anasema Nassibu.

Mwandishi wetu anafuata maelekezo ya Nassibu ya kuandika barua kwenda kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na Mkurugenzi wa Jiji na siku kadhaa baadaye, anaenda kuonana na mkurugenzi wa manispaa ambaye naye, anamuelekeza kwenda kukutana na Afisa Afya wa Manispaa ya Kinondoni, Mathias Nemes Kapizo.

Kapizo kimsingi ndiyo msimamizi wa shughuli zote za kiafya wilayani humo na pia ndiye anayeratibu na kusimamia maiti zinazozikwa na manispaa.

OFISINI KWA AFISA AFYA WA MANISPAA

Baada ya kufika ofisini kwa Kapizo, alitoa ushirikiano mzuri kwa mwandishi wetu na yafuatayo ni maelezo aliyoyatoa kulingana na maswali aliyokuwa anaulizwa:

Swali: Ni maiti za namna gani zinazozikwa na manispaa?

Kapizo: Hapa huwa tunashughulika na maiti zisizokuwa na ndugu, maiti za ajali ambazo zimeharibika kiasi cha kutotambulika na zile zinazotokana na magonjwa hatari kama Ebola, Kipindupindu na magonjwa mengine kama hayo.

Nyingine ni zile zilizotelekezwa na ndugu zao hospitalini. Unakuta mgonjwa ametoka kwa mfano Kigoma, kabla ya kufikishwa Dar es Salaam, ameshapitia kuanzia kwa waganga wa kienyeji na kwenye hospitali mbalimbali ambako kote alikuwa akitoa fedha.

Mtu wa namna hii, unakuta ndugu zake wameshatumia fedha nyingi sana mpaka akija kufika kwenye hospitali za hapa, ndugu wanakuwa wameishiwa. Kwenye hospitali zetu za serikali si unajua mgonjwa akilazwa anatakiwa kulipia kila siku?

Na kama ikitokea amefariki, ndugu hawawezi kupewa maiti mpaka wawe wamelipa deni, sasa wengi wakifikia hatua hii, huwa wanakimbia na kutelekeza maiti wodini kwa kuwa wanakuwa hawana fedha za kulipa deni wala za kusafirisha. Maiti za namna hii huwa tunazizika pia.

KUHUSU WANAOKUFA KWA KIPINDUPINDU, EBOLA

Swali: Ni tahadhari gani huwa mnazichukua mnapozika maiti za watu waliokufa kutokana na magonjwa hatari kama Ebola na Kipindupindu?

Kapizo: Hakuna kazi ngumu kama hiyo kwa sababu kitaalam, maiti ya aina hiyo haitakiwi hata kuingizwa mochwari, madaktari wakishathibitisha amekufa ni moja kwa moja anatakiwa kwenda kuzikwa.

Tahadhari ni kuvaa mavazi maalum ya kuzuia uambukizo na kuhakikisha watu wasiohusika hawasogei kabisa kwenye eneo la mazishi. Changamoto kubwa katika hili huwa ni vifaa vya kutendea kazi, yakiwemo mavazi maalum na madawa ya kujikinga.

Swali: Kwa wastani mnazika maiti ngapi kwa mwezi?

Kapizo: Siwezi kusema ni maiti ngapi kwa sababu siku zinatofautiana, kukiwa na ajali nyingi au magonjwa ya milipuko huwa tunazika wengi lakini siku ambazo hayo hayapo, kwa wastani huwa ni maiti tano hadi sita kwa mwezi.

KUHUSU UDHALILISHAJI WA MAITI

Swali: Yapo madai kwamba maiti zisizo na ndugu huzikwa zaidi ya moja kwenye kaburi moja na wakati mwingine, nyingine hukatwa miguu au mikono ili zote ziingie kwenye kaburi moja. Unalizungumziaje hili?

Kapizo: Hakuna kitu kama hicho hata kidogo. Hao wanaozusha maneno hayo, wanapaswa kupimwa akili zao. Ndugu mwandishi, mfano mwepesi tu, huko barabarani si kila siku huwa unaona mizoga ya wanyama kama mbwa na wengine? Je, umewahi kuona mzoga wa mbwa unakatwa miguu kisha ndiyo unafukiwa?

Itaendelea wiki ijayo.

Leave a Comment