×

Kisa wivu, amnyonga mkewe mjamzito gesti

gestiGesti aliponyongewa.

Na: Gabriel Ng’osha na Mayasa Mariwata,  RISASI Mchanganyiko

INAUMA SANA! Mapenzi ni jambo hatari zaidi katika maisha ya binadamu kuliko kitu kingine chochote. Hii ni kwa sababu, mtu anaweza kufanya ukatili mkubwa kwa mtu aliyekuwa kipenzi chake, wakishiriki pamoja kwa kila jambo, ikiwa ni pamoja na kuzaa watoto.

Hivi ndivyo ilivyomtokea Hadija Shabani, mwanamke mwenye umri wa miaka 21, ambaye wiki mbili zilizopita alikorofishana na mumewe, Dickson Adamu aliyezaa naye mtoto mmoja wa kike, huku tumboni akiwa na ujauzito wa miezi nane.

Katika mzozo huo, unaodaiwa kuwa siyo wa kwanza, wawili hao walitengana, wakagawana walichochuma pamoja kisha kila mmoja akachukua hamsini zake, mke akaenda kuishi maeneo ya Manzese Big Brother, kwa dada yake ili kujipanga upya.

Lakini wiki mbili baada ya tukio hilo, Dickson alifika nyumbani kwa mzazi mwenzake na bila shaka kumpa vishawishi vya hapa na pale, vilivyomlainisha Hadija na kumuamini mumewe wa zamani, hivyo kukubali kwenda kulala naye katika nyumba ya kulala wageni iliyo jirani na wanapoishi, iitwayo Jodam.

Kumbe Dickson hakuwa na mapenzi ya kweli na mkewe na alienda kwake akiwa na dhamira mbaya moyoni. Akamfanya alichomfanya, lakini siku zote mtu mwovu huishia pabaya. Akiamini baada ya kumnyonga atakuwa hajafa, akatoka nje na kuita Bajaj kisha akampakia mkewe hadi Hospitali ya Palestina iliyopo Sinza.

Pale akawadanganya madaktari kuwa haelewi kilichomsibu mkewe, lakini alidhani ni kifafa cha mimba. Madaktari hao wakamchukua na kuanza kumfanyia vipimo, ambavyo vilionesha Hadija alikuwa ameshafariki, lakini ni baada ya kubaini alama za vidole vilivyomnyonga shingoni mwake.

Wakawatonya polisi waliomkamata Dickson ambaye amehifadhiwa katika Kituo cha Polisi Urafiki, akisubiri kukamilishwa kwa taratibu za sheria ili afikishwe mahakamani.

Dada wa Hadija, Sabeth Shaban amesema kifo cha mdogo wake huyo aliyezikwa Upareni kimemsikitisha sana na kuomba sheria ifuate mkondo wake dhidi ya mtuhumiwa.

Kutoka kwa Mhariri: Tujihadhari sana na wapenzi wetu tuliokorofishana nao. Wengine wana uwezo wa kuficha hasira zao, wakaja kama marafiki kumbe wanataka kukudhuru!

Leave a Comment