Mafanikio hayawezi kuja wakati umelala. Hutakiwi kuuamini sana msemo wa ‘kulala maskini na kuamka tajiri’. Ili ufanikiwe, unatakiwa ufanye kazi kwa bidii.
Leo hii unapomzungumzia Steve Jobs, utakuwa unamzungumzia mtu aliyeleta mabadiliko makubwa duniani katika masuala ya kompyuta. Inawezekana ukawa unatumia iPad lakini hujui mwanzilishi, fahamu kwamba huyu jamaa ndiye mvumbuzi wa iPad ndipo wengine wakavumbua tablets.
Mama yake Clara (Mmarekani) na baba yake Paul (Msyria), hawakuwa watu wenye fedha wala elimu kwani hawakwenda shule. Jobs alipozaliwa tu mwaka 1955, wazazi wake walikubaliana mtoto wao aasiliwe, kweli ikawa hivyo, Jobs akaasiliwa na watu waliokuwa na elimu kubwa waliokuwa wakiishi hapohapo San Francisco nchini Marekani.
Maisha yake nchini Marekani yalikuwa ya tabu, watu waliomuasili hawakuwa na kiasi kikubwa cha fedha.
Baadaye alianza shule hapohapo San Francisco, miaka ya 1960, alijiunga na Shule ya Homestead iliyokuwa California, Marekani, baada ya kumaliza, alijiunga na Chuo cha Reed mwaka 1972.
Wakati maisha yakiendelea, aliamua kuondoka Marekani na kwenda India, hakuwa na fedha hivyo alitaka kupambana kivyakevyake, maisha yake huko yakawa ni kuokota chupa za soda na kwenda kuziuza.
Kutokana na elimu ya kompyuta aliyokuwa nayo, akaona njia nyepesi ya kufanikiwa ni kuanzisha kompyuta zake mwenyewe. Ilikuwa kazi kubwa kwani hakuwa na fedha za kutosha, alichokifanya ni kuangalia udhaifu ulipo, akaangalia kompyuta zinazotumia ‘window’ ambazo zipo chini ya Microsoft, akagundua kwamba zinashambuliwa sana na virusi, hivyo alichokifanya ni kuanzisha kompyuta zake ambazo hazitakuwa zikishambuliwa na virusi, kweli akafanikiwa, akazileta iMac chini ya kampuni yake ya Apple.
Alipata upinzani mkubwa sokoni, alipokosolewa, alijirekebisha, hakutaka kurudi nyuma, aliyaona mafanikio makubwa mbele yake hivyo ilikuwa ni lazima kupambana kila siku.
Baada ya kompyuta zake kufanya vizuri sokoni, akaamua kutambulisha simu zake za kisasa aina ya iPhone. Baadaye aliwaita vijana wake (wenye uwezo mkubwa wa kufikiri (genius) na kuwaambia wafikirie namna ya kutengeneza kompyuta isiyokuwa na ‘keyboard’, walifikiria lakini wakachemka na kuona haiwezekani, ila baadaye yeye mwenyewe aliamua kufikiria na kuja na kompyuta inayoitwa iPad ambapo wengine wakaiga na kutoa tablets.
Jobs aliona ‘laptop’ ni nzito, lazima awarahisishie watu mzigo akagundua iPad zilizoleta mabadiliko makubwa na kumuongezea utajiri.
Jobs alifariki dunia mwaka 2011 na kuacha utajiri mkubwa wa dola bilioni 10.2 (zaidi ya trilioni 20.4) ambapo mpaka mwaka jana ulifikia dola bilioni 19 (zaidi ya trilioni 38).