Mjumbe wa nyumba kumi wa eneo hilo, Ramadhani Urembo akionesha eneo la kisima ambapo mtoto huyo alikutwa amekufa.
Richard Bukos na Issa Mnally, UWAZI
DAR ES SALAAM: Mtoto Leyla Salum (4) aliyekuwa akiishi na wazazi wake, Mtoni Kijichi Kata ya Mwanamtoti jijini Dar, aliyetoweka nyumbani kwao kwa muda wa siku nne, amepatikana akiwa amekufa ndani ya kisima cha maji.
Akizungumza juu ya utata wa kifo hicho, mjumbe wa nyumba kumi wa eneo hilo, Ramadhani Urembo (pichani) alisema walimtafuta mtoto huyo kwa muda wote baada ya kupotea bila mafanikio.
“Miongoni mwa sehemu tulizomsaka ni zile hatarishi kama vile kwenye madimbwi, vichaka na majumba mabovu na tulikwenda hata pale tulipomkuta, lakini hatukumuona.
“Tena tulipokwenda pale kwenye lile shimo, siku hiyo maji yalikuwa shida, yalichotwa yote. Tangu apotee Alhamisi mpaka Jumamosi tulikuwa tukimsaka na kwenye shimo hilo tulienda mara kadhaa bila kumuona, lakini cha ajabu Jumapili tukapata taarifa kuwa mtoto yuko kwenye shimo hilo.
“Hali hiyo imetupa mshangao mkubwa sana, yaani kila mtu anashangaa na kusema hapa kuna jambo, haiwezekani pale mahali tumepakagua kwa siku tatu bila kuona chochote, lakini siku inayofuata tumkute mtoto yuko pale.
“Ule mwili ulivyotolewa mimi nilikuwa mmoja wa tuliopanda gari la polisi kwa ajili ya kwenda kuufanyia uchunguzi, lakini wakati nikiwa karibu haukuwa na harufu wala dalili yoyote kuonesha kama ulikuwa na siku nne kwenye shimo hilo,” alisema mjumbe Urembo.
Shuhuda mwingine aliyezungumza na gazeti hili aliyejitambulisha kwa jina la Husna, alisema watoto kupotea mtaani hapo limekuwa ni jambo la kawaida, kwani baadhi hupatikana na wengine hawapatikani.
Shuhuda huyo aliomba jambo hilo lifanyiwe kazi kwani wamekuwa wakiishi kwa mashaka na watoto wao.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Kamishna Msaidizi wa Jeshi hilo, SACP Gilles Muroto alithibitisha kutokea tukio hilo na kuwataka wananchi wanaohisi utata wowote, waende ofisini kwake ili kuwapa mwanga wa kuanza uchunguzi.
“Nani anasema kuna utata? Kama kuna mtu yeyote anaona tukio hilo lina utata aje hapa ofisini kwangu aeleze utata aliouona tuufanyie kazi, na siyo kuongelea mitaani, sisi hatufanyii kazi maneno ya mitaani,” alisema.