Uwazi labaini ukweli hoteli Dar kufungwa! - Global Publishers

Imewekwa na on July 19th, 2016 , 08:13:38am

Uwazi labaini ukweli hoteli Dar kufungwa!

43Mkurugenzi wa Miradi, Uwekezaji na Mipango wa NSSF, Yakoub Kidula

Na Hashim Aziz, UWAZI

Dar es Salaam/Pwani: Kufuatia wimbi la hoteli kubwa na baa maarufu nchini kufungwa huku wamiliki wengine wakiamua kubadili biashara, yamezuka madai mengi mitaani, wengine wakihusisha kutetereka huko kwa wafanyabiashara na kuingia madarakani kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Uwazi limechimba kwa undani na kuja na ukweli wa sakata zima.

mwanzaJB BELMONT HOTEL

Miongoni mwa hoteli zilizofungwa ni pamoja na hoteli maarufu za JB Belmont, mbili zilizokuwa jijini Dar es Salaam na nyingine iliyokuwa jijini Mwanza ambapo mwandishi wetu alifunga safari mpaka ilipokuwa moja ya hoteli hizo, Jengo la Benjamin Mkapa, Posta Mpya.

Katika utafiti wake, Uwazi lilibaini kuwa hoteli hiyo na nyingine zinazomilikiwa na mmiliki huyo, zilifungwa katikati ya mwaka 2015 (kabla JPM hajaingia madarakani), huku chanzo chetu kikieleza kwamba licha ya kufungwa milango, samani nyingi za thamani zilikuwa bado zipo ndani ya majengo hayo kwa maelezo kwamba zimeshikiliwa na NSSF (Shirika la Hifadhi ya Jamii), wamiliki wa jengo hilo.

Ili kujiridhisha zaidi, mwandishi wetu alimtafuta afisa uhusiano na mawasiliano wa NSSF ambaye naye alimuelekeza mwandishi wetu kuonana na Mkurugenzi wa Miradi, Uwekezaji na Mipango wa NSSF, Yakoub Kidula.

Kidula alikiri kufungwa kwa hoteli hizo ambazo mmiliki wake alikuwa mpangaji wao kwa madai kwamba alikuwa akidaiwa fedha nyingi (kati ya shilingi bilioni mbili hadi tatu) za kodi ya pango na alishindwa kulipa kama mkataba ulivyokuwa unamtaka.

“Tulilazimika kumuondoa kwenye majengo yetu ya Dar es Salaam na Mwanza na kushikilia mali zake mpaka atakapolipa deni lakini naona hakuridhika na uamuzi wetu, akaenda kutufungulia kesi mahakamani, hivi tunavyozungumza bado kesi haijatolewa hukumu,” alisema Kidula.

kiromo-view-resort-hotelKIROMO VIEW HOTEL

Uwazi lilifunga safari mpaka ilipokuwa hoteli ya kitalii ya Kiromo View, kilometa 54 kutoka jijini Dar es Salaam na takriban kilometa 10 kutoka Bagamoyo ambapo mwandishi wetu alishuhudia hoteli hiyo ambayo ilikuwa maarufu sana, ikiwa imegeuka ‘gofu’, nyasi nyingi zikiwa zimeota hadi getini huku mbuzi na wanyama wengine wa kufugwa wakionekana ndani ya eneo la hoteli hiyo. Uwazi lilifanya jitihada za kuingia eneo hilo bila mafanikio kwani hakukuwa na mtu yeyote, zaidi ya kuwepo dalili za walinzi ambao nao hawakuwepo kwa wakati huo.

Katika nusanusa yake, Uwazi lilifanikiwa kukutana na mmoja kati ya waliokuwa wafanyakazi wa hoteli hiyo ambaye alikataa kutaja jina lake gazetini, aliyedai kwamba hoteli hiyo ilifungwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) baada ya kubainika kwamba haikuwa ikilipa kodi kama inavyotakiwa.

“Rais Magufuli alipoingia tu, ndiyo ikafungwa lakini nasikia tayari bosi yupo kwenye mchakato wa kubadilisha eneo hili litumike kwa kazi nyingine. Kwa kweli sisi tuliokuwa tukifanya kazi hapa tumeathirika sana, mimi kama unavyoniona, nilikuwa naendesha maisha kwa kutegemea hii kazi lakini sasa hivi nauza mkaa. Kwa kweli hali ni mbaya,” alisema.

LANDMARK HOTELLANDMARK HOTEL

Hii ni miongoni mwa hoteli zilizofungwa hivi karibuni ambapo taarifa za ndani, zinaeleza kwamba mmiliki wake ambaye ni mbunge kwenye serikali ya JPM (jina kapuni), ameamua kubadilisha biashara.

“Ndiyo kama hivi, tulipewa tu taarifa kwamba sisi wafanyakazi tutafute kazi nyingine maana hoteli inafungwa kwa sababu inajiendesha kwa hasara, si unajua mambo ya kodi haya! Nilikuwa nalea familia nzima kwa kufanya kazi hapa Landmark, hata sijui nitaishije,” alisema mfanyakazi mmoja aliyeomba hifadhi ya jina lake.

Omary Mbuli, meneja wa hoteli hiyo, alinukuliwa akisema hawezi kueleza sababu kubwa iliyofanya bosi wake aamue kubadilisha biashara, kutoka hoteli hadi hosteli ya wanafunzi wa vyuo na kutaka atafutwe mmiliki mwenyewe au viongozi wa juu.

Juhudi za kuwatafuta viongozi wa juu wa hoteli hiyo au mmiliki, ziligonga mwamba kutokana na simu zao kutopatikana hewani lakini taarifa zisizo rasmi, zinaeleza kwamba mmiliki ameamua kubadilisha biashara baada ya hoteli hiyo kushindwa kujiendesha kwa faida, makato ya kodi yakiwa makubwa huku idadi ya wateja nayo ikipungua kwa kasi.

Aidha, baa maarufu nazo zimekumbwa na hali hiyo miongoni ni Maryland iliyopo Mwenge ambayo imefungwa kutokana na kilichoelezwa na afisa mmoja wa TRA kuwa ni malimbikizo ya kodi ya mapato yaliyofikia shilingi milioni 139.

 Mkurugenzi wa Umma wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo (pichani) alisema kufungwa kwa baa hiyo ni kazi ambayo  itakuwa endelevu nchi nzima kusaka wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi.

 

Tupia Comment Yako, Matusi Hapana

Stori zinazo husiana na ulizosoma