Nelly Mwangosi mshindi wa nyumba akishuka kwenye basi na familia yake wakati alipowasili Kituo cha Mabasi Ubungo jijini Dar jana kwa ajili ya kukabidhiwa nyumba leo.
HATIMAYE Nelly Mwangosi, aliyeibuka mshindi wa droo kubwa ya Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba, iliyoendeshwa na Global Publishers Ltd kwa muda wa miezi sita, jana aliwasili jijini Dar akitokea nyumbani kwake Iringa na leo atalala Salasala ulipo mjengo wake wenye thamani ya mamilioni ya shilingi.
Nelly Mwangosi akiwa na familia yake.
Nelly ambaye ni mama wa watoto wawili mwenyeji wa mkoani Iringa, aliibuka kidedea katika droo ya mwisho iliyochezeshwa Mbagala Zakhem, jijini Dar es Salaam Juni 30, mwaka huu na kuhudhuriwa na mamia ya wasomaji wa magazeti ya Global Publishers, ambayo ni Championi, Ijumaa, Risasi, Amani, Uwazi na Ijumaa Wikienda.
Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho alisema jana kuwa mambo mengine yote muhimu kuhusu makabidhiano hayo ya nyumba yamekamilika na kwamba mshindi huyo atapewa nyumba yake hiyo leo katika hafla ya makabidhiano itakayofanyika saa sita mchana.
“Tuliahidi na lazima tutekeleze, kama tulivyosema hapo nyuma, tumedhamiria kwa dhati kabisa kurejesha kidogo tunachokipata kwa wasomaji wetu ambao wametoa mchango mkubwa kwa kampuni yetu kwa kipindi chote cha uwepo wake. “Mtakumbuka hii siyo mara ya kwanza kwa sisi kuandaa bahati nasibu kama hii, tumeshafanya hivyo mara nyingi na leo haiwezi kuwa mara ya mwisho.
“Tutaendelea na mpango huu, mwisho wa bahati nasibu hii ni mwanzo wa bahati nasibu nyingine, ninachopenda kuwafahamisha wasomaji wetu ni kwamba wakati wowote tutawaletea kitu kingine ambacho kitakuwa ni chenye manufaa kwao, tunaomba waendelee kutuunga mkono,” alisema meneja huyo.
Droo ya shinda nyumba ilianza Desemba mwaka jana kwa kuhusisha droo ndogo nne ambapo wasomaji walijishindia zawadi ndogondogo nyingi zikiwemo pikipiki, vyombo vya jikoni, mashuka, tv flat screen na vingine vingi.
Nelly mwenye umri wa miaka 45, ambaye amekuwa msomaji wa magazeti pendwa ya Global Publishers kwa zaidi ya miaka 18, wakati akifahamishwa kuhusu ushindi wake, alisema hiyo ilikuwa ni bahati nasibu yake ya kwanza kushiriki licha ya kampuni kuwa nazo nyingi, zilizohusisha magari ya aina mbalimbali, pikipiki, televisheni na kadhalika.
“Nilipopigiwa simu ya ushindi, sikumuambia mtu yeyote kwa kuwa sikuamini, nilimwambia mume wangu pekee na kukubaliana kusubiri kuona nini kingeendelea, nilipoona jina langu limeandikwa gazetini kuwa ni mshindi ndipo nikaanza kuwaambia ndugu zangu, nimefurahi sana kwa kweli,” alisema mshindi huyo, ambaye hakuwahi kuwa na ndoto za kumiliki nyumba jijini Dar es Salaam.
Nyumba atakayokabidhiwa mshindi huyo yenye vyumba vitatu, sebule, jiko, bafu na choo ina samani za kisasa ndani yake, kitu kitakachomfanya kuingia na kuanza maisha pasipo na haja ya kununua fenicha mpya.
Video: Mshindi wa Nyumba Atua Dar kwa Kishindo


