×

Siri Nzito Arusha: Wasichana Wawili Wapotea Kwa Zaidi ya Mwaka – Video

Wasichana wawili wa jijini Arusha, Karen Mark Didas (23) na Nakivona Toroka (22), ambao hawajaonekana kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Wasiwasi umeendelea kuongezeka kufuatia kupotea kwa wasichana wawili wa jijini Arusha, Karen Mark Didas (23) na Nakivona Toroka (22), ambao hawajaonekana kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Tukio hilo limeibua mjadala mpana mtandaoni huku familia, marafiki na umma wakitaka majibu ya haraka kutoka kwa vyombo vya usalama.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, mtu anayedaiwa kuwa na ukaribu na Karen, Godwin Ndosi, amesema mara ya mwisho kuwasiliana na Karen ilikuwa tarehe 21 Juni 2025 kupitia ujumbe mfupi wa simu, ambapo Karen alimweleza kuwa anaelekea Namanga kumsindikiza rafiki yake Nakivona kwenda kuonana na mpenzi wake.

Tangu hapo, simu ya Karen haikupatikana tena. Godwin amesema alishauriwa kutoa taarifa polisi, lakini awali hakuchukuliwa maelezo kwa kile kilichoelezwa kuwa ukosefu wa viashiria vya tukio la uhalifu na nafasi yake kama rafiki.

Ameongeza kuwa alilazimika kufuatilia suala hilo kwa zaidi ya siku 10 kabla ya kuchukuliwa maelezo na maafisa wa upelelezi kutoka Ofisi ya DCI Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa za awali za uchunguzi, rekodi za mawasiliano zinaonyesha kuwa mara ya mwisho wasichana hao walionekana katika eneo la Namanga siku ya tukio.

Hata hivyo, hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa tukio la uhalifu uliothibitishwa hadi sasa.

Wakati huo huo, Godwin amedai kuwa taarifa zilizosambaa mitandaoni zimemharibia taswira ya biashara yake, huku akidai kupokea vitisho mbalimbali.

Aidha, amesema baadhi ya watu wanaohusiana naye, wakiwemo meneja wa biashara yake na dereva, wamekamatwa na polisi kwa ajili ya mahojiano, pamoja na baba yake kuitwa kituoni, licha ya yeye mwenyewe kutodaiwa rasmi na vyombo vya usalama.

Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea huku mamlaka zikihimizwa kuongeza juhudi za kuwatafuta wasichana hao na kutoa taarifa sahihi kwa umma.

Ripoti kamili ya tukio hili inapatikana kupitia Global TV.

Imeandaliwa na Mwandishi Msomi @Korumba_Lebabazi.

🔴 Tufuatilie kupitia YouTube ya Global TV, like, comment ili kuendelea kuhabarika kila siku kwa habari mbalimbali zenye ukweli na uhakika.

Leave a Comment