Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji (kushoto) akiongea.
Wilbert Molandi, Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji, amewatangazia wanachama wake kuwa, kutakuwa na mkutano mkuu wa timu hiyo utakaofanyika Jumamosi hii, Agosti 6, mwaka huu.
Hiyo ni siku chache tangu Klabu ya Simba ifanye mkutano wake mkuu pamoja na wanachama wake na kufikia baadhi ya makubaliano ikiwemo kuboresha mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit, mkutano umepangwa kufanyika kuanzia saa 3:00 asubuhi kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Deusdedit alisema wanachama wote hai waliolipia kadi zao za uanachama, wameombwa kujitokeza kwa wingi ili kufanikisha mkutano huo.
Aliongeza kuwa, siku hiyohiyo ya Jumamosi watakuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.
“Ninaomba nichukue nafasi hii kuwatangazia wanachama wote wa Yanga kuwa Jumamosi ya wiki hii kutakuwa na mkutano mkuu wa klabu yetu utakaofanyika Diamond Jubilee.
“Pia, Jumamosi hiyohiyo, timu yetu ya Yanga itacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa,” alisema Deusdedit.

