×

TFF yamkataa Omog Simba

IMG-20160623-WA0002-1

Kocha Mcameroon, Joseph Omog wa Simba.

Khadija Mngwai, Dar es Salaam

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema kuwa hadi sasa linamtambua Kocha wa Azam FC, Mhispania, Zeben Hernandez, kufuatia kupokea kibali chake cha kufanya kazi nchini huku wakiwa hawatambui uwepo wa kocha Mcameroon, Joseph Omog wa Simba kutokana na kibali chake kutowasili katika shirikisho hilo.

TFF pia imezitaka klabu zote za ligi kuu kuwasilisha nakala tatu za usajili wa kila mchezaji ili kuweza kutambuliwa kabla ya kuupitisha usajili huo.
Akizungumza na Championi Jumatano, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, amesema kabla dirisha la usajili halijafungwa, klabu zote zinatakiwa kuwasilisha vibali vya usajili wa wachezaji ili vihakikiwe na iwapo kibali cha mchezaji yeyote hakitafika, basi hatapata nafasi ya kucheza. Alisema kwa upande wa makocha wamepokea vya makocha wa Azam pekee.
“Tumeamua kutumia kanuni ya 67 kifungu cha 1, 2 na 8 katika kuhakikisha klabu zote za ligi kuu zinawasilisha nakala za usajili wa wachezaji wao ambapo zinatakiwa kuwa tatu na kila mchezaji wa ligi kuu atalipiwa kiasi cha shilingi 50,000 na wa Ligi Daraja la Kwanza shilingi 25,000.
“Kwa upande wa makocha, hadi leo kocha ambaye kibali chake kimewasili hapa TFF ni wa Azam pekee pamoja na Obrey Chirwa, mchezaji wa Yanga na dirisha la usajili litafungwa Agosti 6, mwaka huu.
“Upande mwingine, timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys inaelekea Afrika Kusini kesho (leo) baada ya mechi yake na Madagascar waliyojipima leo (jana) kwa ajili ya mchezo wake wa Jumamosi na kisha mchezo wa marudiano utakuwa tarehe 21 mwezi huu katika Uwanja wa Chamazi na mwalimu ameelezea kuwa anaendelea kuinoa safu ya ushambuliaji.
“Lakini pia kozi ya makipa wa timu za taifa na ligi kuu imeanza Jumatatu na makipa 26 wananolewa. Kozi inaitwa Advanced Coach, itakuwa ya siku tano na itamalizika siku ya Ijumaa, baadhi ya makocha wanaopata kozi hiyo ni pamoja na Mwalami Mohamed, Juma Pondamali, Elyutery Mholery na Salehe Ahmad wa Zanzibar Heroes,” alisema Lucas.

Leave a Comment