Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akizungumza jambo katika hafla hiyo.
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye, jana Ijumaa alizindua rasmi kituo cha Televisheni cha TV1 Tanzania kuanza kurusha matangazo ya moja kwa moja ya mpira wa miguu ya Ligi Kuu Soka ya England ‘EPL’ matangazo ambayo yanatarajia kurushwa kuanzia leo Agosti 13, mwaka huu.
Nape akijibu swali la mmoja wa wahudhuriaji wa hafla hiyo juu ya mechi hizo zitakazoanza.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency zamani The Kilimanjaro Mkurugenzi wa Kituo cha TV 1 Tanzania, Joseph Sayi alisema hii ni fursa kubwa kwa wadau wa soka hapa nchini kuishuhudia ligi hiyo moja kwa moja ambayo ni ligi inayopendwa na kufuatiliwa na Watanzania walio wengi.
Waziri Nape akiwa katika mahojiano ya moja kwa moja na studio za TV 1 zilizoko Mikocheni wakati wa uzinduzi huo.
Alisema Ligi kuu soka nchini England ndiyo ligi maarufu zaidi duniani na hiyo kutokana kushirikisha timu kongwe zenye ubora na mashabiki dunia nzima kama Manchester United, Liverpool, Arsenal pamoja na Chelsea.
Waziri Nape akimkabidhi king’amuzi cha Star Times, Balozi Paul Rupia kwenye hafla hiyo.
Sayi aliongeza, TV1 Tanzania ndio kitakuwa kituo pekee cha runinga hapa nchini kupewa haki za kurusha matangazo hayo yatakayokuwa ‘live’ yakihusisha pia uchambuzi wa ligi hiyo ambapo kutakuwa na vipindi vya kabla ya mechi na baada ya mechi husika.
Naye mgeni rasmi wa uzinduzi huo, Waziri Nape alisema kwa niaba ya serikali anaona fursa hiyo itakuwa ni chachu kubwa kwa michezo ya hapa nchini na kuwashukuru TV 1 kwa kuwa katika kiwango cha kimataifa maana ni hatua ya kipekee kuonesha mpira ‘live’ na Watanzania waitumie fursa hiyo vyema katika vipindi hivyo.
Baadhi ya wageni waalikwa wakifuatilia hafla hiyo iliyokuwa ikiendelea ukumbini hapo.
Baadhi ya watangazaji na wachambuzi watakaokuwa wakishiriki katika urushaji wa matangazo hayo na uchambuzi ni Ally Kashushu na Dkt. Leakey Abdallah ambaye ni mchambuzi mwenye uzoefu wa miaka 20 kwenye tasnia ya michezo husasani uchambuzi.
Shughuli hiyo ikiendelea ukumbini hapo.
Mchambuzi wa Michezo, Dk. Leakey wakati wa hafla hiyo na TV 1 ilifanya mahojiano ya moja kwa moja ambapo alisema Watanzania wategemee uhondo wa ligi hiyo kutokana na uwepo wa wachezaji nyota na makocha mahiri kama Antonio Conte, Arsene Wenger, Jurgen Klopp na makocha hasimu Jose Mourinho wa Manchester United na Pep Guardiola wa Manchester City.
Tv1 Tanzania ni kituo cha runinga kichoanza mwaka 2013 ambapo kilianza kurusha matangazo yake rasmi Januari 2014 ambapo kimekuwa kikiandaa na kurushwa vipindi vyenye ubora wa hali ya juu ambapo TV 1 inapatikana kupitia ving’amuzi vya StarTimes namba 103.
Mkurugenzi wa Kituo cha TV 1 Tanzania, Joseph Sayi (aliyopo mbele) akizungumza jambo.
Denis Mtima/GPL
