Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Leticia Mosore, akizungumza na wanahabari leo.
ALIYEKUWA Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Leticia Mosore, amesema hatambui kusimamishwa kwake na kuvuliwa uanachama na mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia, huku akidai kuwa Mbatia ameshindwa kusimamia chama chake na badala yake anakalia malumbano.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Mosore alisema hajaelezwa sababu za kuvuliwa cheo na kusimamishwa uanachama kwani hata barua aliyopewa haikueleza vifungu vya katiba au kanuni zilizotumiwa na chama hicho kufikia uamuzi huo.
Mosore akisikiliza maswali yaliyokuwa yakiulizwa na wanahabari.
Amesema amesimamishwa uanachama na kuvuliwa cheo kinyume cha katiba ya chama hicho ibara ya 10 (4) ya mwaka 1992 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2014 inayompa mwanachama nafasi ya kujitetea mbele ya kikao cha chama hicho kinachohusika katika mashtaka au madai yoyote na kinampa haki ya kukata rufaa kwenye vikao vya juu iwapo hakuridhika na uamuzi wa kikao cha chini.
“Sikuitwa kwenye kikao hicho kama mtuhumiwa ili kuweza kujitetea na wala sikupewa siku kumi na nne za kujieleza kwa maandishi kama katiba ya chama inavyosema. Mwaliko niliopata ulikuwa ni barua ya kuhudhuria kikao kama makamu mwenyekiti ambaye ni mjumbe wa halmashauri kuu ya taifa,” alisema.
Wanahabari wakichukua taarifa kwenye hafla hiyo.
Aidha aliituhumu halmashauri kuu ya chama hicho kwa kutumiwa na mwenyekiti Mbatia kufikia maamuzi kinyume na katiba ili kutengeneza tuhuma dhidi yake kwa kuanzisha mashtaka kwenye kikao hicho na kufikia maamuzi bila ya yeye ambaye ni mhusika kusikilizwa au kujitetea.
BARUA YA KUMSIMAMISHA UANACHAMA
NA DENIS MTIMA/GPL
