×

Serikali Kuwalinda Watoa Taarifa Za Uhalifu

1.Mkurugenzi Msaidizi Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria,Kamana Stanly (kushoto) akiwa na Mkuu wa Kitengo Cha Mawasilianno Serikalini, Shaiba Bulu.

Mkurugenzi Msaidizi Utekelezaji wa Katiba kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Kamana Stanley akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu kuanza kutekelezwa kwa Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi ya mwaka 2016 inayolenga kuimarisha utawala bora na mapambano dhidi ya uhalifu nchini. Kulia kwake ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa wizara hiyo Sheiba Bullu.

Wanahabari wakichukua tukio hilo.

Serikali  imeanza kutekeleza Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi ya
mwaka 2016 (The Whistleblower and Witness Protection Act. 2016) ili kuimarisha
utawala bora na mapambano dhidi ya uhalifu nchini.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Msaidizi Utekelezaji wa Katiba kutoka Wizara ya
Katiba na Sheria, Bw. Kamana Stanley wakati akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaam kuhusu kuanza kutumika kwa sheria hiyo.

Stanley amesema kuwa  kuwepo kwa sheria hiyokutasaidia kuwapatia ulinzi wa kisheria wale wote wanaotoa taarifa za uhalifu
wa makosa ya aina mbalimbali wanayoshuhudia yakitendeka. Vilevile itarahisisha
utoaji na upatikanaji wa taarifa za uhalifu kwani sasa taarifa hizo zitatolewa
na kupokelewa sio tu kwenye vyombo vya dola pekee bali pia kupitia vyombo vya
habari na vyanzo vingine vinavyobainishwa katika sheria hiyo.

“Wananchi wasiwe na woga kujitokeza kutoa taarifa za uhalifu na matendo ya aina zote yanayofanywa kinyume cha sheria kwani taarifa hizo zitakuwa siri na zitafanyiwa kazi bila ya kuwataja watoa taarifa. Pia mashahidi wanapotakiwa kufika mahakamani wasiogope kwani sheria hii inawalinda” amesema Stanley.

Amefafanua kuwa wahusika watakaoshindwa kushughulikia vyema taarifa zinazotolewa kwao na kuruhusu watoa taarifa na mashahidi kupata madhara, sheria hiyo imeweka utaratibu wa namna ya kushughulika nao.

Aidha, Stanley ameeleza kuwa katika sheria hiyo wale ambao taarifa zao zitafanikisha kuokoa mali ya umma, kupatikana kwa wahalifu na kulinda mazingira na maisha ya
binadamu kutokana na uhalifu uliopangwa kufanyika, wamewekewa utaratibu wa
kupatiwa motisha ikiwa ni pamoja na kuwafidia wale ambao wataathirika kutokana
na taarifa walizotoa.

Stanley ameongeza kuwa Serikali inatarajia kwamba kutungwa kwa sheria hii kutaleta matokeo chanya katika kupambana na uhalifu wa aina zote hivyo kukuza ari ya wananchi kusimamia wenyewe juhudi za kujiletea maendeleo.

“Masuala ya usimamizi wa utawala wa sheria yataimarika kutokana na kuwepo kwa utayari wa wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya uhalifu kwa kufika katika vyombo vya sheria kutoa ushahidi. Pia ushiriki wao katika kufichua maovu yakiwemo
yanayosababisha hasara kwa taifa utasaidia kuinua uchumi ukizingatia kwamba
sasahivi Serikali inapambana sana na mafisadi” ameeleza Stanley.

Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi ya mwaka 2016 (The
Whistleblower and Witness Protection Act. 2016)imeanza rasmi kutumika Julai Mosi
mwaka huu baada ya kuidhinishwa na Waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe.

Leave a Comment