BONIPHACE NGUMIJE, IJUMAA:
MWISHONI mwa mwaka 2014, niliwahi kubahatika kuhudhuria shoo ya Bendi ya Furaha iliyokuwa chini ya Mohamed Amon katika Hoteli ya Kunduchi Beach jijini Dar. Katika shoo hiyo kulikuwa na wakali wengi wa kuimba na kupiga vifaa vingine vya muziki. Kilichonivutia zaidi ni uwepo wa mkongwe wa kupiga saxophone ‘Mdomo wa Bata’ Akualike Salehe a.k.a King Maluu.
Moses akipuliza saxophone kwa hisia kali.
King Maluu aliwahi kubamba na bendi kibao za Muziki wa Dansi kama Maquis de Zaire, Orchestra Safari Sound na Wazee Sugu. Jamaa huyu ni hatari kwa kupiga Mdomo wa Bata na ukitaka kulijua hilo sikiliza ladha yake kwenye Ngoma ya Number One ya Diamond au Tupogo ya Ommy Dimpoz.
Ukiachana na King Maluu, lulu mpya imeibuka katika kizazi hiki cha wapiga Midomo ya Bata. Hapa namzungumzia mkali anayesumbua kwa sasa ndani na nje ya Bongo kwa kupiga Mdomo wa Bata, Moses Zamangwa.
Moses ambaye ni kijana wa makamo, ni mmoja kati ya wapiga Midomo ya Bata waliojizolea umaarufu kwa kupiga shoo nyingi kwenye kumbi, makanisa na sherehe mbalimbali. Akiwa na Vipaji Band, Moses ameshapiga shoo kibao kwa kutumia Midomo ya Bata ambapo ameshaenda nchi kama Indonesia, Qatar, Uturuki, Ujerumani, Swaziland, Ufaransa, Australia na nyinginezo.
Kwa sasa anatamba na albamu yake iitwayo Yote Kwa Yesu yenye nyimbo nane ambazo ni Bwana Mungu Nashangaa, Liko Lango, Nitwae Hivi Nilivyo, Jina Lake Yesu ni Tamu, Karibu na Wewe, Ni Tabibu wa Karibu, Uje Unisaidie na Yote Namtolea.
Hivi karibuni, Moses alitimba ndani ya Global Publishers na kupokelewa moja kwa moja na Global TV Online ambapo alifanyiwa mahojiano katika Kipindi cha Mtu Kati. Katika makala haya anafunguka zaidi;
Global TV: Umeweza kuvuka boda hadi Bara la Ulaya, kule kuna wapigaji wazuri wa Midomo ya Bata, vipi unapata nafasi ya kuwa mtu kutoka Tanzania kwenda kupiga Mdomo wa Bata kule?
Moses: Ujue ni chalenji, ukifika kule unakutana na watu wanaokuzidi kupiga Mdomo wa Bata lakini uzuri ni kwamba ladha ya Afrika ni ya Afrika tu kwa hiyo hata kama kiwango chao kinanizidi ni mimi ndiyo nilikuwa najua siyo wao.
(Anachukuwa Mdomo wa Bata wake na kupiga Wimbo wa Nothing Gonna Change My Love For You wa Gerry Goffin kisha mahojiano yanaendelea…)
Global TV: Unaposafiri kwenda nje, hii ndiyo ladha unayopiga au wao wanataka upige ladha yao kwani ndiyo wanaoijua na kuiamini?
Moses: Inategemea, kuna kipindi unakutana na jukwaa ambalo linahitaji ladha za kwao lakini pia kipindi kingine unakutana na watu wanaotaka kusikia ladha kutoka Afrika hivyo unajigawa nusu kwa nusu.
Global TV: Hebu tufafanulie, unapokwenda Ulaya unakuwa peke yako kutoka Tanzania na unawezaje kupiga hizo nyimbo peke yako?
Moses: Tunaenda kutoka Afrika, mfano Tanzania tunaweza kutoka watu wachache, Afrika Kusini, Ghana, Ethiopia kote watu wachache na tukikutana huko tunaanza kufanya mazoezi kwanza kabla hatujaanza kazi ili tuwe vizuri.
Global TV: Labda hapa nchini wanakulipaje na unapata nafasi ya kupiga sehemu zipi na zipi?
Moses: Watu wengi hawajui kuwa kupata kipato siyo lazima usafiri kwenda nje, hata hapa kuna fursa na inategemea umejipangaje na watu wanakufahamu vipi? Mfano hapa bado sijafahamika sana zaidi ya makanisani ila kuna baadhi ya makampuni huwa wananitumia sana kuburudisha kwenye sherehe zao.
Pia nimetoa CD ya albamu yangu ya kwanza na ni mtu wa kwanza Tanzania kutengeneza albamu ya dini iliyotumia saxophone yenye nyimbo za vitabuni. Pia ukisikiliza redioni nasikika kupitia saxophone kwenye vipindi vingi kama Chombeza Time (Radio One) na vinginevyo. Kwa Tanzania najiona mtu wa kipekee kufanya yote hayo.
Global TV: Kuna mpiga Mdomo wa Bata yeyote ambaye anapiga Mdomo wa Bata mkongwe aliyekuwa kivutio kwako?
Moses: Wapo wengi kama kuna mwalimu wangu huko mwanzoni alinionesha hiki kinashikwa hapa, hiki hapa, anaitwa Rashid Pembe lakini baadaye akaja Tanzania Mzungu kutoka Australia anaitwa Grand, alikuwa kwa muda nikajifunza miaka miwili kwake.
Wapiga Midomo ya Bata Tanzania wapo, namkubali sana King Maluu.
HUYU NDIYO MOSES MDOMO WA BATA, ABURUDISHA BONGO MPAKA MAMTONI
