Nyota wa Man United, Wayne Rooney akifanya yake.
LEO kuna mechi ya watani wa jadi wa Jiji la Manchester yaani ‘Manchester Derby’. Huu ni mchezo unaozikutanisha timu mbili za jiji moja ambazo ni Manchester United na Manchester City.
Nyota wa Man United, Wayne Rooney ndiye mchezaji anayeongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi tangu alipoanza kucheza mechi hizi, kwani hadi sasa amefunga mabao 11.
Ikumbukwe mechi hizi za Manchester Derby ilianza kuchezwa Novemba 12, mwaka 1881 ambapo kwa wakati huo, West Gorton ambayo sasa ndiyo Man City ilifungwa mabao 3-0 na Newton Heath ambayo sasa ndiyo Man United.
ROONEY MKALI WAO
Rooney mwenye umri wa miaka 30, tangu mwaka 2004 ameichezea Man United mechi 371 na kufunga mabao 179 ambayo kati ya hayo, 11 ameifunga Man City na leo anatarajiwa kuiongoza Man United pia akiwa kama nahodha wa kikosi.
Kwa wachezaji wanaocheza sasa, Rooney anafuatiwa kwa ufungaji na Sergio Aguero wa Man City mwenye mabao nane, hata hivyo Aguero leo hatocheza kwani anatumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu.
Wengine wanaofuatia kwa ufungaji ni Joe Hayes na Francis Lee wa Man City wote wana mabao 10, Bobby Charlton wa Man United mabao tisa. Colin Bell wa Man City, Eric Cantona, Brian Kidd na Joe Spence (wote Man United) wana mabao nane.
GIGGS KAPIGA NYINGI
Nyota na kocha msaidizi wa zamani wa Man United, Ryan Giggs anaongoza kwa kucheza mechi nyingi za Manchester Derby akiwa amecheza mechi 36.
COLE, TEVEZ WAPIGA KOTEKOTE
Kama ilivyo kwa Simba na Yanga hapa nchini, kuna wachezaji wamewahi kucheza Man United kisha Man City au kuanzia Man City halafu Man United.
Miongoni mwa wachezaji hao ni Brian Kidd, Andrei Kanchelskis, Peter Schmeichel, Andy Cole, Carlos Tevez na Owen Hargreaves.
Pia wachezaji waliocheza timu mojawapo baadaye wakaenda kuwa makocha upande makocha upande mwingine, hao ni Matt Busby aliyecheza Man City kati ya mwaka 1928 hadi 1936 halafu akafundisha Man United mwaka 1945–1969 na 1970–1971.
Steve Coppell na Mark Hughes hawa walicheza Man United halafu wakafundisha Man City. Hughes alifundisha Man City kati ya mwaka 2008 na 2009.
