×

Rais Magufuli; ‘Katiba ya Warioba’ Ndiyo Jibu!

magufuli

KWA Mtanzania yeyote — hususan kiongozi wa umma — mwenye nia ya kuona furaha, uadilifu na amani vikisambaa katika nchi hii ni lazima ataachana na mchakato wa ‘Katiba Iliyopendekezwa’ na kurejea katika Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inajulikana mitaani kama ‘Katiba ya Warioba’.

Hivi ndivyo Rais John Magufuli, ambaye ameonyesha uadilifu tangu siku ya kwanza kuingia Ikulu, anatarajiwa na Watanzania afanye. Asiwafurahishe wanafiki.

Mfano ‘mbichi’ kabisa wa uadilifu wake ni aliouonyesha majuzi kwa kumpeleka ‘First Lady’, Janeth Magufuli, kutibiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili badala ya kumpeleka hospitali za ‘bei mbaya’ au nje ya nchi kabisa.

Alipuuza tabia ya watangulizi wake waliojua kulikuwa na ‘mafedha ya kumwaga’ ambayo yangeendelea kuwapo hadi siku ya ‘Ufunuo’. Hii ni licha ya viongozi hao kusifia utendaji ‘mzuri’ wa hospitali hiyo.

Wakati Watanzania waadilifu wakimwomba Mungu arejeshe roho njema za viongozi wa nchi hii kwenye rasimu ya Katiba ya Warioba, inasikitisha kwamba washiriki wa tume ya Warioba waliozunguka nchi nzima kukusanya maoni ya wananchi wenzao, wanaonekana kukaa kimya. Huenda wamegundua kwamba kazi yao yote ilikuwa ni kumpigia mbuzi gitaa.

Hata hivyo, pamoja na kimya chao, Watanzania waadilifu na Mwenyezi Mungu, watawapa asante ya milele kwa kuonyesha upendo kwa wananchi wenzao wa leo na wale ambao watazaliwa miaka milioni moja ijayo, kwani walifanya kazi ambayo huenda ilisimamiwa na malaika kutoka mbinguni!

Kitu kilichowashangaza hata malaika ni kwamba, pamoja na wajumbe wengi wa tume hiyo kuwa na kadi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) mifukoni mwao, bado walizishinda hisia zao, wakaja na rasimu iliyozingatia matakwa ya ‘wana wa Adam’ wote wa Tanzania.

Kitu cha ajabu zaidi katika mchakato huo, ni ajali mbaya ya makusudi pale rais mstaafu Jakaya Kikwete alipoongoza vita dhidi ya rasimu hiyo, akauteka mchakato mzima, akayatupilia mbali mambo mengi muhimu yaliyopendekezwa, mengine yakachakachuliwa ili kuyapunguza nguvu au kuyaongezea ugumu ili yasitekelezeke!

Mheshimiwa Kikwete alifanya hivyo licha ya kwamba yeye ndiye aliyeituma tume hiyo na kuipa mabilioni ya fedha. Matokeo yake, kile kilichokuja kuibuka kwa jina la ‘Katiba Inayopendekezwa’, ni andiko la CCM lililopitishwa na wanachama wake kwa shangwe za Kiduku na Singeli.

Rais Magufuli aliyepania kupiga vita matumizi mabaya ya raslimali za umma, kujenga uadilifu hususan kwa viongozi na kusimamia haki za wananchi hususan maskini, hatasita kurejesha macho na mioyo ya Watanzania katika ‘Katiba ya Warioba’, katiba ambayo ingerahisisha zaidi kazi yake na kumfanya awe shujaa wa Watanzania wote kama ataipitisha akingali madarakani.

Katiba ya Warioba imejaa kila aina ya silaha za uadilifu, hekima, busara, huruma, haki na uwazi ambazo zingempa kiongozi jasiri wa aina ya Magufuli nguvu zote zenye dhamira njema ya kuleta furaha kwa wakazi wote ambao Mungu aliwapa nchi ya Tanzania.

Kwa viongozi wenye dhamira za kujijenga wao na jamaa zao leo tu, wakasahau kwamba hawatakaa madarakani milele, wakapuuza pia maslahi ya watoto na wajukuu zao, wakapuuza pia na nguvu za usomi wao, Katiba ya Warioba ilikuwa na inaendelea kuwa tishio na ‘mtoto mbaya’ kwao, ndiyo maana waliitupilia mbali na kuandika katiba inayokidhi matakwa yao – Katiba Inayopendekezwa!

Watanzania wanaoipenda nchi hii leo na miaka milioni ijayo, wanamwomba na kumwambia Rais John Joseph Pombe Magufuli kwamba: “Katiba ya Warioba ndiyo jibu!”