DAR ES SALAAM: JESHI la polisi nchini limewataka wamiliki wa kumbi za starehe kuzingatia uhalali, matumizi na usalama wa kumbi hizo kulingana na uwezo wake kuhusu idadi ya watu.
Hayo yamesemwa leo na Kamishna Msaidizi wa Polisi Makao Makuu, Advera Bulimba, alipozungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam hususan katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya.
Kamishna Msaidizi wa Polisi Makao Makuu, Advera Bulimba akizungumza na wanahabari.
Bulimba pia alizungumzia ushirikiano wa jeshi hilo na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vilivyojipanga katika kipindi hiki cha sikukuu hizo ili kuhakikisha wananchi wanazisherehekea kwa amani na utulivu bila kuwepo na vitendo vyovyote vya uhalifu.
“Ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu,’’ alisema.
Wanahabari wakimsikiliza Bulimba wakati wa mkutano huo.
Aidha jeshi la polisi limetoa tahadhari kwa wananchi wote kuwa makini na kuchukua hatua stahiki za haraka kwa kutoa taarifa kupitia namba za makamanda wa polisi wa mikoa na namba za zisizokuwa na malipo za 111 na 112 pindi watakapoona viashiria vyovyote vya uharifu katika maeneo mbalimbali.
“Hali kadhalika wamiliki wa maduka makubwa tunawakumbusha kufunga kamera za CCTV ili kurekodi mienendo ya watu wanaoingia na kutoka katika maduka yao kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali ili kubaini uhalifu na wahalifu kwa haraka,” aliongeza.
Na Denis Mtima/GPL