Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga
Dar es Salaam: Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, limesema litahakikisha linapambana na madereva wanaovunja sheria za usalama barabarani kwa makusudi, ili kudhibiti ajali ambazo huwa zinaongezeka katika kipindi cha Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake, Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga, amesema jeshi lake halitawavumilia madereva wanaoendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa, wanaoyapita magari mengine (overtake) bila kufuata sheria, wanaoendesha magari kwa kasi kubwa na wasiozingatia sheria za usalama barabarani, huku akiahidi kuwa baadhi ya madereva watafungwa jela badala ya kulipishwa faini kama ilivyozoeleka.
Maofisa mbali mbali wa jeshi la polisi wkifuatilia mkutano huo.
“Katika kipindi hiki, watu wengi hupenda kusafiri kwenda maeneo mbalimbali na hivyo kuongeza matumizi ya vyombo vya moto barabarani. Kipindi hiki huambatana na starehe nyingi ikiwa ni pamoja na ulevi kwa madereva… na hatimaye kusababisha ajali ambazo hugharimu maisha ya watu wengi.
“Tumejipanga vizuri ili kuwatia mbaroni madereva wote watakaokiuka sheria za usalama barabarani na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema kamanda Mpinga.
Na Denis Mtima/ GPL.




