×

Farid Mussa: Najua ugumu nitakaoukuta Hispania

farid-mussa-12

  • Asema Yanga walinifuata nikawaambia lengo langu ni kucheza Arsenal

Omary Mdose na Ibrahim Mussa, Gazeti la Championi Ijumaa, Desemba 30, 2016

JUZI Jumatano usiku, kiungo wa Azam FC, Farid Mussa, hatimaye alikwea pipa kuelekea Hispania kujiunga na timu ya Tenerife inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini humo.

farid-mussa-6

Kiungo huyo anajiunga na timu hiyo kwa mkopo wa miaka miwili akitokea Azam FC baada ya kufuzu majaribio Mei, mwaka huu.

Alikwama kusafiri kwa takribani miezi sita akihangaikia kibali cha kufanyia kazi Hispania.

Championi Ijumaa lilizungumza naye akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere muda mfupi kabla ya kuondoka nchini.

Kabla ya mahojiano hayo, Farid aliwasili uwanjani hapo akiwa na mama yake, ndugu zake wawili na rafiki zake watatu, huku kukiwa hakuna kiongozi yeyote wa Azam.

farid-mussa-1-001

Umejipangaje kwa ushindani?

“Najua kuna mtu anayecheza nafasi yangu lakini kwa kuwa wameniita basi wameona nipo vizuri kuliko aliyepo. Nimejipanga kupambana kwa kila hali na namuomba Mungu anipe subira kwani najua lazima nitapata shida kabla ya kuzoea mazingira.

farid-mussa-33Hali ilikuwaje ulipokuwa hujapata kibali?

“Nilikua najihisi vibaya lakini kuna watu walikuwa wakinipa moyo, mmoja wao ni (Mbwana) Samatta. Unajua Samatta ni mmoja kati ya wachezaji wanaopenda maendeleo hasa katika taifa lake, awali wakati Tenerife walipotaka kuninunua moja kwa moja huku Azam wakitaka niende kwa mkopo, akawa ananiambia mdogo wangu ‘usilazimishe sana kuondoka na wala usikubali kubaki Tanzania, baki na msimamo wako wa kuondoka lakini lazima ukubaliane na klabu yako’.

“Amenisaidia sana, kila viongozi wa Azam waliponiuliza nikawa nawajibu jinsi ambavyo Samatta amenielekeza.

Ikafikia kipindi Azam wakajua kweli nina malengo ya kucheza soka nje ya nchi na si kubaki Tanzania, wakaanza kunisaidia na mpaka leo hii nimetimiza lengo langu.

Nini siri ya mafanikio yako?

“Hakuna zaidi ya nidhamu, siku zote soka linaendana na nidhamu ya nje na ndani ya uwanja.

farid-mussa-34

Aandaliwa programu maalum

“Kwa sasa Tenerife wapo katika kipindi cha mapumziko na ndiyo maana wameniambia niwahi na tayari kuna programu maalum wameniandalia ili ligi ikiendelea niwe tayari nimeshazoea mazingira pamoja na mfumo, nadhani itanichukua wiki moja au mbili kukopi kila kitu.

“Nakumbuka mara ya kwanza nakwenda kufanya majaribio Mei, mwaka huu, wiki ya kwanza niliumwa mafua pamoja na homa, lakini baadaye baada ya kuzoea hali ikawa sawa.

farid-mussa-35Azam imewatimua makocha wao, unazungumziaje hilo?

“Ni makocha wazuri labda hawakuwa na bahati ya kufundisha soka hapa Tanzania lakini walifanikiwa kwa kiasi fulani kuibadilisha Azam.

“Pia miundombinu haikuwa rafiki kwao, ikawafelisha, ukiangalia viwanja vya kule kwao na walivyovikuta huku ni tofauti kabisa, ikawa shida kwao na kushindwa kufanya kazi yao kwa ufanisi mkubwa.

Watanzania wengi wakienda nje wanarudi na visingizio vingi, umejipangaje kwa hilo?

“Binafsi siwezi kumzungumzia mtu, lakini mimi sifikirii kurudi Tanzania kucheza soka, malengo yangu ni kufika mbali zaidi ya Tenerife na siku moja nije kuwa mmoja kati ya Mtanzania nitakayeisaidia nchi yangu.

Yanga walimtaka, akawachomolea

“Wakati wa usajili wa dirisha dogo lililofungwa hivi karibuni, Yanga walikuwa wananihitaji sana tu baada ya kuona dili la kwenda Tenerife kuchelewa, katibu wao (Baraka Deusdedit) alinipigia simu na kunieleza hilo niliwaeleza kuwa bado nina mkataba na Azam, na malengo yangu ni kucheza nje ya Tanzania na si hapa tena.

Nashukuru walinielewa, unajua ndoto yangu kubwa ni kuichezea Arsenal au Atletico Madrid.

Awaachia viatu Agyei, Mahundi

“Naondoka lakini najua kuna wachezaji wataziba pengo langu, yupo Enock Atta Agyei na Joseph Mahundi ambao wamesajili hivi karibuni, naamini hao ndiyo watachukua nafasi yangu.

Neno kwa wachezaji wa Azam

“Nawaambia wasibweteke, wazidi kupambana kwa ajili ya timu na kuifikisha mbali zaidi ya ilipo sasa.

Anawaambia nini Watanzania?

“Waniombee niweze kufanikiwa ili kuitangaza zaidi nchi yetu, kwangu inaweza kuwa njia kwa wengine kufuata.”

YANGA 4 – 0 NDANDA FULL TIME (MAGOLI YOTE)