×

Bilionea jay z anakutaka uuanze mwaka kwa tamaa ya mafanikio!

Jay+Z+Tops+Cardigan+F50_EPAliMFxMakala: Nyemo Chilongani na Mtandao, Gazeti la Ijumaa, Toleo la Januari 02, 2017

Tumeumaliza Mwaka 2016 tukiwa bado na ndoto za kufanikiwa na kuwa kule ambapo kila mmoja anataka awepo. Kwa mwaka uliopita, tumewaona mabilionea wengi wakituelezea siri zao za kufanikiwa. Kama umekuwa mfuatiliaji mzuri wa ukurasa huu, wengi wametuambia vitu vilevile ambavyo nina imani kama tukivifanyia kazi hakika tutafanikiwa.

Tunapouanza mwaka 2017, ni vizuri tukazingatia somo kutoka kwa bilionea ambaye ni Mwanamuziki wa Marekani, Shawn Carter ‘Jay Z’ kujua alikopitia kabla na baada ya kupata ubilionea. Ni mwanamuziki mkongwe, mwenye mafanikio makubwa, mwenye kampuni yake ya kutengeneza nguo ya Rocawear na pia akiwa amekwishawahi kuimiliki Timu ya Mpira wa Kikapu ya Brooklyn Nets hadi mwaka 2013.

Unapomzungumzia Jay Z au Jigga huyuhuyu unayemuona akifokafoka runingani, utakuwa ukimzungumza mmoja wa wanamuziki matajiri zaidi duniani akiwa anashika nafasi ya pili nyuma ya Sean Combs ‘P Diddy’ (figa ambayo hubadilika mara kwa mara). Utajiri wake unatajwa kufikia dola milioni 610 (zaidi ya shilingi trilioni 2.5.)

Kila Jay Z anapohojiwa runingani amekuwa akiwasisitiza kuhusu kufanikiwa. Amekuwa akiwaambia kuwa, kuna raha ya mtu kuwa bilionea kama yeye. Baadhi ya mambo hayo ni haya hapa;

 beyonce-jay-z.jpg

FANYA BIASHARA UNAYOIPENDA

Jay Z anasema: “Kufanya biashara unayoipenda ndiyo siri ya mafanikio yangu. Huwa siwezi kuanzisha biashara ambayo sitakuwa na furaha kuifanya. Niliamua kufanya muziki kwa sababu ndicho kitu ninachokipenda, ninapoifanya, moyo wangu unafurahia na kuifanya kwa moyo wa dhati.

“Niliamua kuanzisha biashara ya kuuza nguo. Ninapenda kuvaa, mavazi yalinipa pesa kubwa katika maisha yangu. Unapoifanya biashara unayoipenda, hata ufuatiliaji wake unakuwa mwepesi kwa kuwa ni kitu ambacho unakipenda kwa moyo wote. “Pia ninawekeza sana katika vilabu mbalimbali vya mchezo wa kikapu. Ninafanya hivyo kwa kuwa ninaupenda mchezo huo. Ni tofauti kabisa na ukiniambia niwekeze katika mchezo mwingine, nitashindwa.”

NEW YORK, NY - MAY 12:  Jay-Z attends the Miami Heat vs Brooklyn Nets game at Barclays Center on May 12, 2014 in the Brooklyn borough of New York City.  (Photo by James Devaney/GC Images)

NI LAZIMA UWE TOFAUTI NA WENGINE

Anasema: “Najua wakati mwingine inaweza kuwa vigumu lakini ukweli ni kwamba ni lazima uwe tofauti na wengine. Huwezi kumuona mtu anafanya biashara fulani na wewe ukaifanya kama yeye, ni lazima uje na muonekano tofauti.

“Nilipoingia kwenye biashara ya muziki, nilijua kwamba kuna watu wakali, kama Ice Cube, Dr. Dre na wengineo. Nilijua kwamba ningekuwa mchanga, watu wasingenikubali ila kama ningetaka watu wanikubali ni lazima nifanye kitu tofauti na wao.

“Nikafanikiwa kuleta ladha tofauti na nikapata mashabiki na mwisho wa siku kuwa hapa nilipo. Kama kweli umedhamiria kufanya biashara ni lazima uhakikishe unakuwa tofauti ndipo utafanikiwa, ila ukitaka kufanya kama wengine, utabaki hapohapo kwani wenzako wataendelea kuwa bora.”

Beyonce-Jay-Z-Best-PDA-Moments-Pictures.jpg

HAKUNA KITAKACHOKUINGIZIA PESA KAMA KIPAJI

Jay Z: “Huu ndiyo ukweli. Matajiri wengi wanaochipukia ni watu wenye vipaji mbalimbali. Ninaonekana tajiri, nataka nikwambie ni kwa sababu ya kipaji changu. Achana na biashara zangu za nguo na vitu vingine, chimbuko la mambo yote ni kipaji changu cha kuimba.

“Unapoamua kuwekeza kwenye kipaji chako, hakika kitakufikisha utakapotaka kwenda. Kwa kuwa leo utaingia kwenye biashara hii na kesho biashara ile kutokana na fedha uliyoipata kupitia kipaji chako. Kuna wengine wamezaliwa kufanya biashara, familia ni wafanyabiashara, ni lazima ujue kwamba hicho kimekuwa kama kipaji chako, kwa hiyo kitu ulichorithi ni lazima ukifanye kwenye ubora mkubwa.”

SHIRIKIANA NA WENGINE

Jay Z anaendelea: “Huwezi kufanikiwa peke yako, ni lazima kuwe na watu ambao utakuwa ukifanya nao biashara ili kufanikiwa. Si lazima wawe wafanyabiashara wenzako, hata wateja unaweza kushirikiana nao na kufanikiwa.

“Wengine huwa wachoyo kwa kuhisi kwamba kama wakishirikiana na wengine basi watafanikiwa wao na yeye hatafanikiwa. Rafiki yangu, kwenye biashara kuna ushirikiano mkubwa sana, leo ningeamua kufanya mimi kama mimi, nisingefanikiwa kabisa, nisingekuwa nimefika hapa nilipokuwa siku ya leo, ukihitaji kufanikiwa huna budi kushirikiana na wenzako.”

RUDISHA KWA JAMII SEHEMU YA ULICHOKIPATA

Jay Z: “Tunafanya biashara kisha tunaiuzia jamii inayotunzunguka, si ndiyo? Basi tunapopata kiasi fulani cha fedha, hatuna budi kuirudishia jamii kiasi kile tulichokuwa nacho. Tutembee watoto yatima na kuwapa zawadi kidogo, tuwatembelee watu wenye matatizo mbalimbali na kuwasaidia.

“Hakuna mtu aliyefilisika kwa sababu ya kutoa sana. Unapotoa, hata Mungu anakuona, anakubariki. Naweza kusema kwamba biashara zangu zinafanikiwa kwa sababu ninatoa kwa jamii. Hakikisha unapokuwa na biashara yako, unapata nafasi ya kutoa kiasi fulani kwa jamii ambayo imekufanya kuwa hapo ulipo.”

Mashabiki Walivyoupokea Mwaka Mpya 2017 kwa Shangwe DAR LIVE