ATIZO la fangasi katika ubongo (Mucormycosis), ni ugonjwa ambao katika siku za hivi karibuni umekuwa maarufu huku ukisababisha vifo vya watu wengi. Kitaalamu, ugonjwa huu husababishwa na fangasi waitwao Murcorales ambao huingia ndani ya mwili wa binadamu kwa njia ya hewa. Ukivuta hewa yenye fangasi hao, huingia na kwenda moja kwa moja kwenye mfumo wa damu kisha kuanza kuzunguka ndani ya mwili kufuata damu.
Baada ya kukaa kwa wiki kadhaa kwenye mfumo wa damu, huhamia kwenye uti wa mgongo (spinal) ambapo huzaliana kwa wingi na kuanza kusambaa kuelekea kwenye ubongo. Fangasi hawa wanapofika kwenye ubongo, huushambulia na kusambaa kwa kasi ambapo uwezekano wa mgonjwa kupona huwa mdogo sana. Kati ya kila watu 100 wenye ugonjwa huu, karibu 30 hupoteza maisha.
DALILI ZA UGONJWA
Dalili za awali za ugonjwa huu ni kuwa na uvimbe mwekundu unaotokea kuzunguka macho ambao huongezeka kadiri fangasi wanavyozidi kushambulia ubongo. Dalili nyingine ni pamoja na kuumwa kichwa upande mmoja, uso kuuma, homa kali, kupumua kwa shida na kutokwa kamasi zenye rangi nyeusi. Pia ngozi ya mwili wa mgonjwa huanza kubadilika rangi na kuwa nyekundu. Hali hiyo huendelea mpaka ngozi inapobadilika zaidi na kuwa nyeusi.
TIBA
Vipimo vya ugonjwa huu hufanywa kwa mashine ya MRI ambapo mtu akibainika ameambukizwa fangasi hawa, hutibiwa kwa upasuaji wa ubongo na kuondoa sehemu zilizoathirika pamoja na kutumia dawa kali za Amphotericin B au Posaconazole, wakati mwingine dawa hizi huchanganywa pamoja.
WATU WALIOPO KWENYE HATARI
Watu wanaoweza kuupata ugonjwa huu kwa urahisi ni wagonjwa wa kisukari, HIV, waliofanyiwa upasuaji wa kupandikiza viungo ndani ya miili yao kama figo au ini, na matumizi ya dawa za ‘corticosteroids’ kwa kipindi kirefu.