×

Ndindi Anaonyesha Njia Kwa Samatta

| CHAMPIONI | LEICESTER, England

KOCHA wa Leicester City, Claudio Ranieri alikubali kumuuza kiungo Ngolo Kante kwenda Chelsea akijua wazi atamsajili Wilfred Ndidi kutoka KRC Genk ya Ubelgiji ili asaidie katika kiungo.

Ndidi raia wa Nigeria Hadi Desemba Mwaka jana alikuwa akiichezea Genk sambamba na Mtanzania Mbwana Samatta japokuwa Desemba 3, 2016 klabu yake ilikubali kumuuza kwa dau la pauni milioni 17 sawa na Sh bilioni 46.4 kwenda Leicester.

Mwanzo zilikuwa tetesi tu lakini Januari 5, mwaka huu, Ndidi alisaini kuichezea Leicester ambayo ni bingwa mtetezi wa Ligi Kuu England ‘Premier’.

Kwa kuwa alisajiliwa kama kiungo, moja kwa moja Ndidi aliingia kikosi cha kwanza na alicheza mechi yake ya kwanza Januari 7, 2017 dhidi ya Everton ambapo Leicester ilishinda mabao 2-1 katika mechi ya Kombe la FA raundi ya tatu.

Januari 14, mwaka huu, Ndidi alicheza mechi ya kwanza ya Premier akiwa katika jezi ya Leicester dhidi ya Chelsea ambapo walipoteza kwa kufungwa nyumbani mabao 3-0.

Mchezo huo ndiyo uliomkutanisha Ndidi na mchezaji aliyemsababisha asajiliwe yaani Kante, hata hivyo hakuweza kuisaidia timu yake mpya kupata ushindi nyumbani.

BAO LAKE LAIVUSHA LEICESTER

Usiku wa kuamkia Alhamisi wiki hii, Ndidi alianzia benchi katika mchezo wa raundi ya nne wa Kombe la FA dhidi ya Derby County kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Kings Power. Mbele ya mashabiki 31,648 ilionekana Ndidi angemaliza akiwa benchi katika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Mike Jones, lakini dakika ya 90 wakati timu zipo sawa kwa bao 1-1, Ranieri aliamua kufanya mabadiliko.

Katika mabadiliko hayo, alimtoa Nampalys Mendy na kumuingiza Ndidi pia alimtoa Ahmed Musa na kumuingiza Islam Slimani. Kabla ya hapo, bao la kwanza la Leicester lilifungwa na Andy King dakika ya 46.

Ndidi aliifungia Leicester bao la pili na la kwanza kwake dakika ya 94 kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Derby, Jonathan Mitchell. Demarai Gray aliifungia Leicester bao la tatu dakika ya 114 na Leicester ikashinda mabao 3-1.

Huo ni ushindi wa kwanza wa Leicester kwenye uwanja wake wa nyumbani mwaka huu na unaonekana kuamsha hamasa ya upambanaji ndani ya kikosi hicho. Kwa ushindi huo, Februari 18, mwaka huu Leicester sasa itacheza na Millwall katika hatua ya 16 Bora ya Kombe la FA.

NAFASI KWA SAMATTA

Genk mara kadhaa imekuwa ikitoa wachezaji kwa timu za Premier hata ligi nyingine kubwa za Ulaya, kitendo cha Ndidi kuanza kufanya vizuri inaweza kuwa njia ya kutoka kwa Samatta.

Klabu za England ikiwemo Leicester yenyewe zitakuwa zimetoa jicho kwa Genk ili kutazama kama kuna mchezaji mwingine wanaweza kumchukua na haiwezi kushangaza kuona Samatta anatazamwa sana.

Kama Samatta akiendelea kufanya vizuri katika kikosi cha Genk kwa kufunga mabao katika kila mechi, ni wazi jicho linaweza kuwa kwake na kupata nafasi ya kusajiliwa England au kokote Ulaya.

WILFRED NDIDI

Onyinye Wilfred Ndidi alizaliwa Desemba 16, 1996 na sasa ana umri wa miaka 20.

Ndidi alizaliwa Lagos, Nigeria na sasa ana urefu wa futi 6 na inchi 2. Ndidi ambaye anavaa jezi namba 25 katika kikosi cha Leicester, alianza soka mapema miaka ya 2000 katika akademi ya Nath Boys hadi mwaka 2015 alipojiunga na Genk.

Aliichezea Genk mechi 61 na kufunga mabao manne hadi Januari mwaka huu alipojiunga na Leicester. Alicheza timu ya vijana ya Nigeria chini ya miaka 20 (U20) kati ya mwaka 2013 hadi 2015.

Ndidi ameichezea Nigeria mechi sita tangu mwaka 2015 na amekuwa akiitwa na kuachwa kikosini hapo.