×

Valentine DaY Hii, Jumuika Mubashara na Mwenza Wako!

 

Na GABRIEL NG`OSHA| IJUMAA WIKIENDA| XXLOVE

VALENTINE DAY hii, jumuika mubashara na wako! NINA kila sababu ya kumtukuza na kumshukuru Mungu kwa sababu ya pumzi aliyonijalia, nawe msomaji shukuru kwa kila hatua na hali unayoipitia katika maisha yako. Mpenzi msomaji wa safu hii ya XXLove, napenda kutumia fursa hii kukutakia kila la heri kwenye siku hii kubwa ya wapendanao au Valentine’s Day ambayo kesho (Jumanne) itakuwa ndiyo inaadhimishwa duniani kote.

Katika siku hii muoneshe umpendaye kwa kujumuika naye mubashara hadi wengine wawaonee donge. Bila shaka kwa wapendanao, huu ni mwezi wao, mwezi wa kung’ara kwa rangi nyekundu, hakika ni jambo zuri la kukutana na kushirikiana kwa wale wote ambao wanapendana kwa dhati.

Lakini ni vyema pia tukakumbuka kuwa, Valentine’s Day si tu kwa wapenzi, bali hata kwa mama, baba, kaka, dada, babu,bibi mwenye nyumba wako, marafiki, wapenzi, wachumba, wanandoa na binadamu wote kwa jumla.

Ni jambo la kupendeza mno la kuoneshana upendo kwa kweli usiokuwa na chembe ya maigizo ndani yake. Kimsingi ni siku ya kumuonesha mwenzako ni kiasi gani unampenda na kumjali katika maisha yako.

Kama kweli unampenda mpenzi wako na mwezi huu wa wapendanao umepanga kutumbua kile ulichonacho, basi utakuwa ni mwanaume au mwanamke mwema na bora zaidi kama utatumbua hivyo vinono ukiwa na mweza wako kuliko kama utatumia nafasi hiyo kutumbua na watu ambao siyo wapendwa wako, bali ni watu tu wa mpito katika maisha yako.

Kwa wapenzi ni muda mzuri wa kuoneshana mapenzi ya dhati kuwa mnapendana.

Ni muda wa kufanya marejeo mapya ya penzi lenu. Kama kuna sehemu mlijikwaa ni muda muafaka wa kukaa sehemu na kuanza kuulizana hapa ilikuwaje mama au baba f’lani, mbona pale ulifanya vile na hivi, ilimradi tu kuwekana sawa na maisha ya upendo kati yenu yaendee.

Hakuna mapenzi yasiyokuwa na migogoro isipokuwa migogoro hiyo inatofautiana kutoka mtu mmoja na mwingine, kikubwa ni kwamba kama mmeamua kuwa pamoja ni vyema mkapata muda wa kuwa mnarekebishana ili muweze kudumu katika uhusiano wenu.

Mnapopata muda wa kuzungumza na kusahihisha mahali mlipojikwaa, kutawafanya muishi kwa upendo wa muda mrefu kwani kila mtu anakuwa hana kinyongo na mwenzake au ndugu yake.

Kuliko kusubiri kuzungumza au kuonesha upendo Siku ya Valentine pekee.

Angalizo: Kwa wote ambao kesho wamepanga kufanya mambo mbalimbali kwa wapenzi wao ikiwemo kutoa zawadi, kwenda kubarizi (outing), shopping na mambo mengine, niwashauri mfanye vitu kwa kiasi. Usikose wiki ijayo kwa mada nyingine tamu. Kama una maoni au ushauri, tembelea ukurasa wetu wa Ijumaa Wikienda kwenye Mtandao Wa Kijamii wa Facebook, Insta:@mimi_na_uhusiano au jiunge na M&U WhatsApp kwa namba 0679 979 785