SHOGA; Valentine hii si ya kula na jirani
Imewekwa na on February 14th, 2017 , 08:41:17am

SHOGA; Valentine Hii si ya Kula na Jirani


Na SOPHIA MA`MDOGO| GAZETI LA UWAZI| LOVE & LIFE

HEYA haye shoga langu la ukwee! Najua ulikuwa ukinisubiria kwa hamu Jumanne ya leo tukutane tena hapa katika uwanja wetu wa kujidaidai, kujiachia kama si kujishebendua upo? Kwanza siyo tunaenda tu shoga yangu hatujuliani hata hali, domo na macho  yamekukaaa, vipi kwanza mzima wewe? Kama ni mzima ni jambo la kumshukuru Mungu ila kama ni mgonjwa pia ni jambo la kuombeana utapona, sawa! Wiki iliyopita niliongea mengi na wewe shoga yangu, tuliongelea kuhusu mwezi huu nikakwambia kuwa huu ni mwezi mahususi, mwezi wa kukaa na mwenzako na kuangalia wapi mrekebishe msonge.

Nilitokwa povu siku ile shoga langu asikwambie mtu, tena siyo la sabuni? Povu la mwendokasi yaani povu la bia, upo? Hiyo yote shoga ilitokana na meseji niliyopata kwa msomaji wangu mmoja ambaye alikuwa akiteseka kwa kunyimwa chakula cha usiku, yaani mumewe tangu mwaka uanze hakijui chakula cha usiku kwake, yeye akirudi nyumbani ameshiba, loo! Shoga mtu wa aina hiyo kama nilivyokushauri, jaribu kuongea naye vizuri kama anaendelea kukunyima basi kimbilia kwa ndugu wakupe ushauri, upo? Leo ni siku mubashara! Baada ya hayo tuelekee kwa kileee, kilichonifanya nikuandikie haya ya leo.

Najua kila mmoja anajua kuwa leo ni siku mubashara, sasa kama hujui siku mubashara mchukue mwenzako na watoto mkaogelee beach, sawa? Shoga achaga ushamba kama siyo undezi, siku kama hii ya leo ndo kuna wale wanaokimbiwa, wanaodanganywa, wanaochekelea kama siyo kulia, umenipata? Utakulaje kwa jirani?

Kwanza shoga yangu usikubali kudanganyika kwa siku kama ya leo, eti ohh nimepata safari ya kikazi ghafla, mara ohh sijui usiku huu tuna kikao cha dharura, yaani siku zote hakijatokea leo kimetokea?

Shoga mwambie haachwi mtu hapa! Usimwache mwenzako akale chakula cha usiku kwa jirani, itakuwa jambo la ajabu sana kama hutaweka ukaribu na mwenzako leo. Mfanyie yale ambayo hata ulikuwa hujawahi kumfanyia zamani.

Mwambie maneno matamu kwa kila atakachokifanya, mkanye na vyakula vya jirani, mwambie kwanza havina mvuto, si vitamu na vingi vimekosa mapishi mazuri, upo?

Kufuli liwe na rangi shoga! Shoga yangu kama ulikuwa hujui basi kitu kingine kikubwa cha kumpa sapraizi huyo mwenzi wako leo ni kumvalia wazungu wanaita red ‘nyekundu’ kila mahali.

Mpigie red kila kona kuanzia mdomoni, kucha hadi kwenye unyayo, upo? Sogea nikung’ate kasikio shoga maana mimi na wewe tena, toka nitoke, kauka nikuvae, tangulia wewe mi niko nyuma yako!

Raha ya valentine ya leo ukiachana na sapraizi, sijui vijizawadi vya maua ni kutoka na mwenzi wako ukiwa red kila kona iwe brauzi, kufuli na vingine vyote we piga red tu, au naongopa? Mtoko sasa Wapo wengine wanachukulia siku hii kama zile sikukuu za kidini ama kitaifa, shoga ngoma haipigwi kwenye disko na mbuzi hata umpigie muziki wa aina gani ataishia kutikisa mkia tu, kiuno hana!

Tena mwingine leo utakuta anachukua ukoo mzima kama siyo familia, hapa yupo mama pale baba mkwe huku watoto huyooo wamevaa nyekundu wote eti wanatoka kupata msosi maalum wa sikukuu ya valentine, shoga uwe unauliza ati!

Unaweza kuweka unga wa ugali kwenye mtindi ukapika, upo?

Mtoko wa leo unaweza kuwakwepa hata watoto, ukamchukua dada wa kazi pembeni ukamweleza kila kitu na kuwadanganya watoto kuwa unaenda kwa ndugu au sehemu ambayo mnarudi muda si mrefu basi mkafanya vitu kwa kujiachia huko!

Badili mazingira Katika sehemu hii unisikilize kwa makini, siyo kubadili mazingira mtu anajua kubadili baa au hoteli, koma wee! Hapa namaanisha usifanye mambo kwa kukariri, kila ukitoka out na mwenza wako basi ni hoteli au baa hiyohiyo, utachokwa sasa ebo!

Shoga yangu leo ni siku muhimu sana ya kubadili mazingira tena kwenda mbali zaidi mkafanye mipango yenu.

Ujue kuna wengine wameshajiwekea kichwani kuwa siku kama ya leo ni kulala tu chumbani wakila chakula kuanzia asubuhi mpaka kesho yake, loo! Wee nawe! Kwa leo naomba niishie hapa, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine tamu zaidi ya hapa!

Usisahau kwa leo kumwambia mwenza wako neno NAKUPENDA, NITAKUPENDA, USINISALITI, CHUKUA ZAWADI HII na utakachopewa chochote hata kama ni mambo yetu yaleee usisahau kusema ASANTE MPENZI!

 

Tupia Comment Yako, Matusi Hapana

Stori zinazo husiana na ulizosoma