Jinsi ya Kuishi na Mpenzi Mwenye Ujauzito Wako!
Imewekwa na on February 17th, 2017 , 06:38:41am

Jinsi ya Kuishi na Mpenzi Mwenye Ujauzito Wako!

Na HASHIM AZIZ| GAZETI LA IJUMAA| MAKALA

UHALI gani mpendwa msomaji wangu, ni matumaini yangu kwamba uko poa na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku. Karibu tena kwenye uwanja wetu huu tujadiliane na kuelekezana kuhusu mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi.

Sote tunaelewa kwamba hakuna kipindi kigumu katika uhusiano wa kimapenzi kama pale mwenzi wako anaponasa ujauzito. Wanawake wengi huwa na mabadiliko makubwa ya tabia, hali inayowafanya wanaume wengi washindwe kujua namna ya kuishi nao katika kipindi hicho kigumu. Unampenda na unataka kumuonesha jinsi unavyomjali lakini mwenyewe hata haelekei.

Kila unachokifanya anakiona kibaya, kila kitu kinamkasirisha, muda wote anakuwa na hasira au kisirani kiasi cha kufanya uione nyumba yako kuwa chungu? Usijali, unapaswa kumuelewa na kumsaidia kwani anakuwa katika kipindi kigumu sana kihisia, kiakili na kimwili.

MFANO HALISI

Jackson, mkazi wa Morogoro alifunga ndoa na mkewe kipenzi miezi michache iliyopita. Tayari mkewe huyo ameshanasa ujauzito lakini mabadiliko makubwa ya tabia zake, yanamfanya Jackson ahisi kwamba huenda mkewe amepata mwanaume mwingine au hampendi tena.

“Kabla hajapata ujauzito, tulikuwa tukielewana na kupendana sana lakini tangu apate ujauzito, nyumba naiona chungu. Ananikaripia kama mtoto mdogo, kila ninachofanya anaona nakosea.

“Anaweza kuniagiza nimletee zawadi kwa mfano matunda lakini jioni nikimpelekea, atayatoa kasoro kuanzia mwanzo mpaka mwisho kisha anaenda kuyatupa, hivi ni haki kweli hii? Kwenye tendo la ndoa ndiyo kabisa hataki hata nimguse.

“Muda mwingine ananiambia nanuka jasho hata kama nimetoka kuoga muda muda huohuo. Naomba ushauri hivi ananipenda kweli huyu?” Bila shaka msomaji wangu umemuelewa vizuri Jackson anachokisema.Kinachomtokea ndugu yetu huyu, ndicho kinachowatokea wanaume wengi, hasa ambao wake zao au wenzi wao wamepata ujauzito wa kwanza.

NINI CHA KUFANYA?

Hakuna kipindi ambacho mwanaume anapaswa kumnyenyekea mwenzi wake, kumjali na kumuonea huruma kama kipindi ambacho ameshika ujauzito. Safari ya miezi tisa kubeba kiumbe tumboni si mchezo, wanawake wenyewe watakuwa mashahidi kwa jinsi safari ya kulea ujauzito mpaka kujifungua ilivyo ngumu.

Katika kipindi hiki, ni kawaida kabisa kwa mwanamke kuonesha mabadiliko makubwa kama nilivyosema hapo awali, hasa kipindi ambacho mimba inakuwa bado changa.

Ni kipindi ambacho anaweza kusema au kufanya jambo lolote bila kujali madhara yake. Anakuwa siyo yeye tena, tayari amebeba mzigo mzito na mtu pekee wa kumfariji ni wewe.

Wapo baadhi ya wanawake wakibeba ujauzito, huwachukia sana waume zao lakini hali hiyo huisha mara tu baada ya kujifungua au ujauzito kuwa mkubwa.

Haina maana kwamba mapenzi yameisha ndiyo maana hakupendi, la hasha. Anakuwa anakupenda sana lakini hali yake ndiyo inayomsababishia awe hivyo.

Huna haja ya kukasirika hata kama atakuwa anakuudhi na kukukasirisha kiasi gani.

Zipo mbinu nyingi za namna ya kuishi na mwenzi wako akiwa katika hali hii bila kusababisha migogoro ya aina yoyote.

Wiki ijayo tutamalizia sehemu ya pili ya mada yetu kwa kuangalia njia hizo. Kwa maoni, ushauri, nicheki kwa namba za hapo juu.

Kwa stori zote kali, Tu-follow

Facebook @Globalpublishers

Twitter @GlobalHabari

Instagram @GlobalPublishers

YouTube @GlobalTVTZ

Tupia Comment Yako, Matusi Hapana

Stori zinazo husiana na ulizosoma