
JAMAA kacheza soka kwa miaka 20 huku akipata mafanikio makubwa, lakini kikubwa cha kumtofautisha na wengi ni kwamba Sol Campbell katika miaka yote hiyo kacheza kwenye klabu za nchini England tu. Campbell, aliyezaliwa Septemba 18, 1974, alikuwa beki wa kati maridadi sana na aliyejitengenezea heshima kubwa mno katika ulimwengu wa soka kwa miaka yote hiyo aliyowafurahisha mashabiki wake.
Kijana huyu aliyezaliwa jijini London na wazazi wa Kijamaica, alijulikana zaidi kwa mafanikio aliyoyapata akiwa na Arsenal aliyojunga nayo akitokea Tottenham Hotspur mwaka 2001. Hatua ya kujiunga na wapinzani wakuu wa Spurs ilisababishwa achukiwe na mashabiki wa timu hiyo hadi leo hii.
Kwa miaka mitano, akiwa amecheza mechi 195 katika Klabu ya Arsenal, Campbell aliisaidia klabu hiyo kutwaa mataji mawili ya Premier na mawili ya FA, ikiwa ni pamoja na mataji mawili kwa mpigo aliyoyapata msimu wa 2001-02.
Lakini usisahau kuwa huyu ni sehemu ya ile Arsenal Isiyofungika kwa maana ya ‘The Invincibles’ ambayo ilitwaa ubingwa wa Premier bila kupoteza mechi yoyote msimu wa 2003–04. Campbell, 42, anakumbukwa pia kwa kufunga bao pekee katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Barcelona, licha ya kuwa klabu yake iliambulia kichapo cha mabao 2-1 mwaka 2006.
Mwaka 2006, Campbell aliweka historia ya kuwa mchezaji pekee kuiwakilisha England katika mashindano makubwa sita mfululizo, akicheza kwenye Euro 1996, 2000 na 2004 pamoja na Kombe la Dunia 1998, 2002 na 2006. Alitajwa katika kikosi bora kwenye Kombe la Dunia 2002 na Euro 2004. Heshima nyingine aliyowahi kuipata kwenye soka ni kuingia kwenye Timu Bora ya Mwaka Chaguo la Wachezaji (PFA) mara tatu (1999, 2003 na 2004). Campbell ambaye kumpita ilikuwa ni kazi kwelikweli, aliichezea timu ya taifa ya England kuanzia 1996 hadi 2007 na katika kipindi chote hicho cha miaka 11 ya soka la kimataifa, alicheza jumla ya mechi 73 na kufunga bao moja.
Gwiji huyu alitangaza kustaafu kucheza soka la kiushindani Mei 2012 akiwa na umri wa miaka 37. MATAJI: Tottenham: Kombe la Ligi: 1998–99 Arsenal: Premier: 2001–02, 2003–04 Kombe la FA: 2001–02, 2002– 03, 2004–05 Ngao ya Jamii: 2004 Portsmouth: Kombe la FA: 2007–08 England: Euro ya U-19: 1993 Tuzo binafsi: Timu bora ya mwaka Premier: 1998–99, 2002–03, 2003–04 Kikosi Bora cha Kombe la Dunia: 2002, 1992–2001 Tottenham 315 15 2001–2006 Arsenal 197 11 2006–2009 P.mouth 111 2 2009 N.County 1 0 2010 Arsenal 14 1 2010–2011 Newcastle 8 0 JUMLA 646 29

Kikosi Bora cha Kombe la Ulaya (Euro): 2004
MAISHA BINAFSI: Kaka yake Campbell, John alifungwa kwa miezi 12 mwaka 2005 kufuatia kumpiga mwanaume mmoja ambaye alisema Sol ni shoga. Mwaka 2008, Campbell alianza uhusiano wa kimapenzi na mbunifu wa mavazi, Fiona Barratt. Walifunga ndoa Julai 17, 2010 huku Sol akiwa na mtoto wa kiume aliyempata katikauhusiano wake uliopita na Janet Tyler. Campbell alikuwa na majumba mawili ya kifahari jijini London na Northumberland lakini Desemba 2015, aliuza jumba lake moja la Northumberland.
ANACHOKIFANYA KWA SASA
Baada ya kustaafu soka, Campbell alijikita katika siasa. Februari 2015 alitangaza nia yake ya kugombea nafasi ya Umeya wa Jiji la London kwa tiketi ya Chama cha Conservative katika uchaguzi wa 2016 lakini bahati mbaya kura hazikutosha kuchaguliwa na chama chake kuwania nafasi hiyo. Hivi karibuni, Januari 30, 2017, Campbell alirejea kwenye mambo ya mpira, baada ya kuteuliwa kuwa msaidizi wa Dennis Lawrence katika kikosi cha timu ya taifa ya Trinidad and Tobago. Kwa hiyo, hivi sasa Campbell ni kocha msaidizi wa Trinidad and Tobago.