×

Pamoja na Matatizo, Wachezaji Yanga SC Waahidi Kuiua Zanaco

GAWilbert Molandi na Musa Mateja | CHAMPIONI| DAR ES SALAAM

LICHA ya wachezaji wa Yanga kutolipwa mishahara ya miezi mitatu, lakini wamepanga kuingia uwanjani kwa nia moja tu pekee ya kuwafunga wapinzani wao Zanaco ya Zambia huku viongozi wao wakishughulikia tatizo hilo. Timu hizo, zinatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Taifa

jijini Dar es Salaam leo katika mechi ya hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Mshindi wa mechi ya leo atafuzu hatua ya makundi na atakayefungwa atashushwa kucheza Kombe la Shirikisho Afrika akicheza mechi mbili za mtoano na timu za huko kuwania kufuzu Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, viongozi wa timu hiyo wanashughulikia mishahara hiyo na wakati wowote wanatarajiwa kulipwa. Aidha, Championi liliwashuhudia wachezaji hao wakifanya kikao cha wao wenyewe mara baada ya kumalizika kwa mazoezi ya mwisho ya timu hiyo yaliyofanyika jana asubuhi kwenye Uwanja wa Taifa. Katika kikao hicho, wachezaji walionekana

kupeana mioyo ya kijasiri huku wakiweka matatizo yao pembeni na badala yake kuhamasishana ili washinde kwenye mechi ya leo kabla ya kurudiana Lusaka, Zambia.

 

“Wachezaji wote tunatakiwa kuungana na tuwe kitu kimoja ili kuipambania timu yetu kwa lengo la kupata mtaji mkubwa wa ushindi kabla ya kurudiana nyumbani kwao.

“Ninaamini kuwa, kama tukishinda mechi hii viongozi watahamasika na kushawishika kutulipa mishahara yetu ya miezi mitatu, hivyo kila mchezaji atakayepata nafasi ya kucheza, basi anatakiwa kupambana ili tushinde mchezo huu,” alisikika mmoja wa wachezaji akizungumza hayo.