
Na NYEMO CHILONGANI| IJUMAA WIKIENDA| MAKALA
BILA shaka unaufahamu mtandao wa kuhifadhi na kuangalia video za nyimbo na matukio mbalimbali duniani, YouTube.
Ni mtandao uliojipatia umaarufu zaidi kwenye eneo hilo tangu miaka ya 2000. YouTube una watembeleaji au watazamaji zaidi ya milioni 50 kwa siku. Kila anayeingia anakuwa na lengo lake katika kuangalia video mbalimbali zilizowekwa katika mtandao huo.

Wamiliki wake wanapiga tu fedha kupitia YouTube. Kuna wengine maisha yao yanaendeshwa na mtandao huu, wanapata mamilioni ya fedha kwa kuwa tu, wamejanjaruka na kugundua kwamba kupiga fedha si lazima uhangaike sana. Hata ukiwa chumbani kwako, ukijipanga, fedha zitakufuata tu.

YOUTUBE ILIVYOANZISHWA
Mtandao wa YouTube ulianzishwa mwaka 2005 kwa sasa, Chad Hurley ana utajiri wa dola milioni 335 (zaidi ya shilingi bilioni 700), Steve Chen ana utajiri wa dola milioni 300… na vijana watatu ambao walikuwa wafanyakazi katika Kampuni ya PayPal, Chad Hurley, Steve Chen na Jawed Karim
Jamaa hao waliuanzisha mtandao huu kama masihara. Kwamba, kuna siku walikwenda kwenye pati ya rafiki yao. Wakiwa kule, wakasherehekea sana kwa kunywa, kula na kuimba.
Katika tukio hilo kuna mtu alirekodi vipande vya video lakini baadaye waligundua kwamba zile video zilitakiwa kuhifadhiwa sehemu kwani kama wangehifadhi kwa CD, kuna siku zingeharibika na hata kama wangezihifadhi katika kompyuta, inawezekana kuna siku virusi vingezitafuna.
Hapo ndipo jamaa hao walipopata idea (wazo) ya kuanzisha mtandao huu. Lakini wazo lao lilinogeshwa zaidi wakati Mwanamuziki Janet Jackson alipokuwa akiimba katika mchezo wa Super Bowl.
Wakati akiendelea, ghafla titi lake moja lilionekana. Jambo hilo liliwashtua watu wengi na kutaka kuliona mara kwa mara kupitia video. Ukiachana na tukio hilo, pia tukio la Tsunami la mwaka 2004 liliwapa motisha zaidi kwani wengi walichukua video lakini watu walipoingia mitandaoni hawakuziona ndipo jamaa hao wakaanzisha rasmi mtandao huu mwaka 2005.
Video mbalimbali zikaanza kuwekwa na video ya kwanza iliyofikisha watazamaji milioni moja ilikuwa ni ya Tangazo la Nike ambalo lilifanywa na Mwanasoka Ronaldinho Gaucho huku video ya kwanza kuwekwa ikiwa ni Me at the Zoo ambayo iliwekwa na Jawed Karim.
GOOGLE WAKAUNUNUA
Baada ya Google kuona mtandao huo una watu wengi, waliamua kuununua kwa dola bilioni 1.65 (zaidi ya shilingi trilioni 3), dili hilo lilikamilika Novemba mwaka 2006.
UTAJIRI WA WAANZILISHI
Washkaji walifanya biashara nzuri sana, walipiga fedha nyingi, kitu ambacho hawakuamini kama kingetokea.
Kwa sasa, Chad Hurley ana utajiri wa dola milioni 335 (zaidi ya shilingi bilioni 700), Steve Chen ana utajiri wa dola milioni 300 ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 600 huku Jawed Karim akiwa na utajiri wa dola milioni 140 ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 280.
NI FUNZO KWETU
Watu wamekuwa na idea nyingi sana vichwani mwao, zimekuwa zikija na kufa mara moja huku hakuna hata moja ambayo wameijaribu. Nisikilize ndugu yangu, hata hawa walikuwa na idea vichwani mwao, lakini wasingeweza kupata fedha kama tu idea hiyo ingekaa vichwani mwao tu.
Waliondoka na kuifanyia kazi. Ndivyo inavyotokea hata kwa mtu anayetaka kufanya biashara f’lani. Inawezekana ukawa na wazo la kuuza chipsi, wazo likawa zuri lakini hutaki kulifanyia kazi, mwisho wa siku wazo hilo linapotea au kuchukuliwa na mwingine na fedha ulizotakiwa kuziingiza ukazikosa.
Ili ufanikiwe, huna budi kuwa kama watu hawa watatu. Usitake kuwa na wazo halafu likakaa tu kichwani mwako, ni lazima ulitoe na kulifanyia kazi.