×

Farid Mussa Kocha Alinipeleka Timu ya Watoto Hispania

“WAKATI natua Hispania kwa mara ya kwanza maisha hayakuwa rahisi hata kidogo kwani nilitakiwa kukaa nje ya kikosi cha kwanza kwa miezi sita mfululizo.
“Muda wote huo nilikuwa najijenga pamoja na kuzoea hali ya mazingira ya huko katika kikosi cha watoto yaani timu B ambapo kocha ndiye alitoa pendekezo la mimi nipelekwe huko.” Hivyo ndivyo anavyoanza kuelezea kiungo wa CDF Tenerife, Mtanzania Farid Mussa.
Farid ambaye ni zao la Klabu ya Azam, ni miongoni mwa wachezaji watatu wa Taifa Stars ambao wanacheza soka la kulipwa barani Ulaya, wengine ni Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji na Thomas Ulimwengu wa AFC Eskelistuna ya Sweden.
Championi Jumatano limefanya mahojiano na kiungo huyo ambaye analitumia vyema guu la kushoto kuhusiana na maisha yake yalivyo tangu alipotua katika kikosi hicho ambacho kinashiriki Ligi Daraja la Kwanza Hispania.

Maisha ya Hispania yakoje?
“Najisikia faraja kwanza kuwepo na kucheza huko Hispania kwa sababu sasa natambulika kama profesheno nikija hapa nchini lakini suala la maisha ni kawaida tu naendelea kuzoea mambo taratibu kwa sababu bado mgeni kule.”

Ushindani wa ligi ya huko ukoje?
“Ushindani ni mkubwa, timu yangu inakusanya wachezaji kutoka mataifa mbalimbali duniani hivyo kufanya suala la kupata namba liwe gumu na mtu inabidi ujiongeze kuhakikisha unacheza.
“Lakini mwanzoni wakati natua sikuwa vizuri kwa sababu sikucheza hapa nyumbani kwa miezi sita, hivyo baada ya kutua kule nikatengewa programu maalum katika kikosi cha vijana ambayo naendelea nayo.”

Malengo yako ni yapi?
“Kwenda mbele zaidi ya hapa Tenerife nilipofika, nasema kwamba hapa sitabweteka na zaidi nitafanya kazi kwa nguvu kubwa niondoke kwenda kucheza sehemu nyingine na hilo linawezekana kabisa.
“Nataka kuiinua Tanzania ijulikane katika ulimwengu wa soka na naamini hilo litafanikiwa japo kwa sasa kuna changamoto ila napigana nazo kufikia wazo langu hilo.”

Unawasaidiaje wachezaji wenzako wa hapa nchini?
“Mara nyingi naongea na wakala wangu kwa ajili ya kuwasaidia wenzangu wa hapa Bongo kwenda kucheza Ulaya kama Ibrahim Ajibu, Simon Msuva na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na kuna muda wakala alikuwa anaziulizia namba za Ajibu.
“Kikubwa na wao wenyewe wawe na hamu ya kucheza soka la nje siyo kubaki ndani kwa ajili ya kulikuza soka letu kwani hatuwezi kuwa na timu nzuri kwa watu wengi kukaa ndani pekee.”

Unaongea na Samatta? Anakwambia nini?
“Ndiyo tunawasialiana na kikubwa ananipa moyo wa kutokata tamaa hata kidogo na nisibweteke hata kama nikikosa namba katika kikosi cha kwanza kwani hata yeye alianza kwa kuingia dakika tano kabla ya mpira kumalizika lakini sasa ni tegemeo katika kikosi cha kwanza.”

La Liga unaionaje kwa ujumla?
“Ni ligi ngumu ikumbukwe hii ndiyo ligi ya pili kwa ushindani baada ya ile ya England sasa kama mtu anataka mafanikio ni lazima afanye juhudi kubwa kutokana na kukusanya wachezaji wenye viwango vikubwa duniani.”

Vipi kuitwa Stars, unajisikiaje?
“Nafurahia kujumuishwa kwenye kikosi hiki kwa sababu hakuna mchezaji ambaye hapendi kuona analitumikia taifa lake pale anapoaminiwa zaidi, nitaendelea kuitumikia kwa nguvu kubwa kila nitakapopata nafasi.
“Mechi za kimataifa zinakujenga zaidi kama mchezaji na zinakuongezea nafasi ya kujiamini na kufanya vizuri pale unapokutana na watu kutoka taifa lingine.”

Kihispania kinapanda?
“Si rahisi kujifunza lugha yao kwa muda mfupi niliokaa huko, mimi naongea Kiingereza na muda mwingi napata shida kuwasiliana na wenzangu katika mambo mengine kwa sababu wao wanazungumza lugha hiyo lakini uwanjani lugha ya kimpira inaeleweka.”

Msosi wao vipi unapanda?
“Daah mwanzoni ilikuwa shida kwa sababu huelewi ni nini wamepika huku, mimi nimeshazoea vyakula vyetu vya nyumbani sasa kule ilikuwa tabu kweli japo sasa havinisumbui hata kidogo,” anasema Farid.