×

Mo Aipasua Kichwa Simba

Na Omary Mdose | CHAMPIONI| DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, amesema kitendo cha kiungo wake, Mohammed Ibrahim ‘Mo’ juzi Jumamosi kutolewa uwanjani kwa kadi nyekundu, kwa kiasi fulani imemtibulia mipango yake.
Mo alitolewa uwanjani dakika ya 76 katika mchezo wa juzi Jumamosi wa nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Taifa, Dar baada ya kumchezea vibaya beki wa Azam, Shomari Kapombe.
Katika mchezo huo uliomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0, Mo ndiye aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 48.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Omog alisema kadi hiyo inamaanisha kwamba hawezi kumtumia mchezaji huyo kwenye mchezo wa fainali, jambo ambalo linamuumiza kichwa kumtafuta mbadala wake ili waweze kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.
“Kiukweli kumkosa mchezaji muhimu kwenye mchezo wa fainali ni wazi imeniumiza kwani nilikuwa na mipango naye lakini ndiyo hivyo tena imeshatokea hatuwezi kuwa naye, hatuna namna ya kufanya.
“Lakini nitahakikisha namtafuta mchezaji sahihi wa kuziba pengo lake, kwani wapo wengi kikosini kwangu na kama ulivyoona alivyotoka yeye, wapo waliocheza nafasi yake na kulinda ushindi wetu,” alisema Omog.

Leave a Comment