
BAADA ya kusimama kwa takriban mwezi mzima, uhondo wa Ligi Kuu Bara unarejea wikiendi hii, mashabiki wengi wakitaka kuona wakongwe wanaochuana kileleni, Simba na Yanga, watafanya nini katika mechi zao. Simba, baada ya kuambulia suluhu katika mchezo wake wa mwisho Aprili 15, mwaka huu dhidi ya Toto African, kabla ligi haijasimama, keshokutwa Jumapili itavaana na African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Kuelekea mchezo huo, Kocha wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, amesema: “Haiwezi kuwa mechi rahisi hata kidogo kutokana na hali jinsi ilivyo kwenye mechi hizi za kumaliza msimu kwa sababu kila timu inatafuta pointi muhimu kujiweka kwenye mazingira mazuri.

“Walitufunga kwenye mchezo wa kwanza, jambo hilo hatutaki kuliona likijitokeza katika mchezo huu, hivyo lazima tushinde ili kujikita zaidi kileleni kutokana na kwamba tunauhitaji ubingwa wa ligi na hatuwezi kuupata kama tukizembea katika mechi zetu tatu zilizosalia.” Timu hizo zilipokutana kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza, Simba ilikubali kichapo cha bao 1-0.
Simba itaingia uwanjani ikisaka pointi tatu ili kuongeza wigo wa pointi dhidi ya Yanga kwani kwa sasa wapo kileleni wakiwa nazo 59, huku Yanga wakiwa nazo 56 lakini wakiwa na michezo miwili mkononi.
Huku Simba ikizihitaji pointi hizo kujiimarisha zaidi kileleni, wapinzani wao nao wanazitaka ili kujinasua na janga la kushuka daraja kwani kwa sasa wanashika nafasi ya 11 wakiwa na pointi 31 wakisaliwa na michezo mitatu kama Simba.

Kocha wa African Lyon, Mkenya, Charles Otieno, alisema: “Tutaingia uwanjani kusaka matokeo ya ushindi kwa sababu tunataka kutoka huku tulipo ili tuwe salama kuepuka kushuka daraja.
” Wakati Simba ikijiandaa kuikabili Lyon, kesho Jumamosi timu ya JKT Ruvu itakuwa na mtihani mzito wa kuikabili Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Endapo JKT Ruvu itapoteza mchezo huo, basi itakuwa ndiyo timu ya kwanza msimu huu kushuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara ikizisubiri nyingine mbili.

Mbali na michezo hiyo, Majimaji ambayo nayo inahangaika kujinasua na janga la kushuka daraja, itakuwa kwenye uwanja wake wa Majimaji uliopo Songea kucheza dhidi ya Mwadui FC, huku Ruvu Shooting ikiwa Mabatini, Pwani kupambana na Kagera Sugar. Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga watawaalika Prisons kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, wakati Azam watapambana na Mbao FC kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar.